1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Uefa, Euro 2012; Uingereza na Ufaransa zapeta

Vigogo vya soka katika bara la Ulaya vilitoka jasho na kutumia ujuzi wao wote kuweza kufuzu katika michezo ya kundi D.Ufaransa iliizibua Ukraine kwa mabao 2-0,wakati Uingereza ikairarua Sweden kwa mabao 3-2.

England's Daniel Wellbeck celebrates scoring his team's third goal against Sweden during their Group D Euro 2012 soccer match at the Olympic stadium in Kiev, June 15, 2012. REUTERS/Alexander Demianchuk (UKRAINE - Tags: SPORT SOCCER)

UEFA EURO 2012 Schweden vs. England

 Licha  ya  mvua  kubwa  iliyonyesha , lakini  ilikuwa  tu inachelewesha  kile  ambacho  ni  dhahiri, ushindi  kwa  Ufaransa ambayo  imewaadhibu  wenyeji  wenza  wa  mashindano  hayo Ukraine  kwa  mabao  2-0,  na  kuifanya  Ufaransa  kupanda  hadi kileleni  mwa  msimamo  wa  kundi  hilo  la  D. Uingereza  ilibidi kutumia  gea  zote  ili  kurejea  kutoka  nyuma  na  kuisambaratisha Sweden  ambayo  ilionyesha  ukaidi  mkubwa , kabla  ya  kukubali mabao  3-2  na  hivyo  kuyaaga  mashindano  haya  ya  Euro  2012.

Mabao  yaliyowekwa  wavuni  katika  muda  wa  dakika  tatu yalitosha  kuiweka  Ufaransa  katika  nafasi  ya  juu, baada  ya mabao  ya  Jeremy Menez  katika  dakika  ya  53  na  Yohan Cabaye kupachika  bao  la  pili  katika  dakika  ya  56  katika  uwanja  wa club  ya  Donetsk  wa  Donbass Arena.

Mvua  yachelewesha  mchezo

Ukraine's Andriy Shevchenko (L) challenges France's Adil Rami during their Group D Euro 2012 soccer match at Donbass Arena in Donetsk June 15, 2012. REUTERS/Michael Buholzer (UKRAINE - Tags: SPORT SOCCER)

Mpambano kati ya wachezaji wa Ukraine na Ufaransa

Anga  la  Ukraine  lilimwaga  maji  muda  mfupi  tu   baada  ya kuanza  mchezo  huo, na  refa  kutoka  Uholanzi  Bjoern Kuipers aliziondoa  uwanjani  timu  hizo  na  kuzipeleka  katika  vyumba  vya kuvalia  vya  uwanja  huo  wa  Donbass Arena ikiwa  ni  chini  ya dakika  tano  tu  baada  ya  mtanange  huo  kuanza.

Wafanyakazi  waliingia  uwanjani  kujaribu  kukausha  maji  katika uwanja  ambao  ulikuwa  umejaa  maji  chepechepe na  refa Kuipers  alianzisha  tena mpambano  huo  baada  ya  kusubiri  kwa  muda  wa  karibu  saa nzima. Ushindi  huo  umeifanya  Ufaransa  kuwa  haijafungwa  katika michezo  23 , na  kukiweka  kikosi  hicho  cha  Les Bleus  kuwa  na points  nne  juu  ya  msimamo  wa  kundi  D wakati  Ukraine  ikibakia na  points  3.

Sweden yaaga  mashindano

Uingereza  imejinyakulia  points  nne  pia   baada  ya  ushindi  wa mabao  3-2  dhidi  ya  Sweden  ambayo  kimsingi  imetolewa  katika kinyang'anyiro  hicho, ikiwa  hadi  sasa  haijapata  point baada  ya michezo  miwili.

Uingereza  haikuonekana  kama  timu  yenye  nidhamu  ambayo kocha  wake  Roy Hodgson  anataka  kuiunda , lakini  ilitiwa  hamasa na  mchezaji  aliyeingia  katika  kipindi  cha  pili Theo  Walcott waliisambaratisha  Sweden  kwa  mabao  3-2  katika  mchezo  wa kuvutia  wa  fainali  za  kombe  la  Euro  2012  katika  kundi  D, na kuifikisha  timu  hiyo  karibu  na   robo  fainali.

Danny Welbeck of England scores their third goal past Andreas Isaksson of Sweden during the UEFA EURO 2012 group D match between Sweden and England at The Olympic Stadium on June 15, 2012 in Kiev, Ukraine. (Photo by Martin Rose/Getty Images) - eingestellt von gri

Danny Welbeck akipachika bao la Uingereza dhidi ya Sweden

Wameonyesha  moyo  na ujasiri  wakati Walcott alipowazindua kutoka  katika  dakika  kumi  za kunyong'onyea ambapo walipambana  kutoka  kuwa  nyuma  kwa  mabao  2-1  na  hatimaye kusawazisha  na  bao  la  kiufundi  la  Danny  Welbeck, lilikamilisha ushindi  wao  waliopata  kwa  kazi  ngumu  na  kuwaondoa  Sweden katika  mashindano  haya.

Kocha akubali wajibu

Kocha  wa  Sweden  Erik Hamren  ametetea  mchezo  wa  timu  yake wa  kushambulia , kwa  kusema  tumeonyesha   jinsi tunavyopaswa  kucheza . Baadhi  ya  nyakati  hatufanikiwi . Naamini  kwa  mtindo  huu  wa  kusakata  soka  tutapata  matokeo mazuri  hapo  baadaye.

Lakini  kwa  bahati  mbaya  tumeathirika  , na  inauma. Tulikuwa  na ujasiri  wa  kucheza  jinsi  tunavyotaka  kucheza, amesema. Lakini kuna  msemo  wa  Kiswidi unaosema , kuwa  operesheni  ilikuwa nzuri  sana  lakini  mgonjwa  amefariki. Hivi  ndivyo  tunavyojisikia . Nachukua  jukumu  la   timu  hii. Nahisi  nina  wajibu  mkubwa kwa  matokeo  haya, amesema  Hemren.

Nae  kocha  wa  Uingereza  Roy Hodgson  amesema  anapanga kumchezesha  Wayne  Rooney  siku  ya  Jumamosi  dhidi  ya Ukraine  katika  mchezo  wa  mwisho  wa  kundi  D, baada  ya ushindi  wa  kazi  dhidi  ya  Sweden. Pia  amewasifu  wachezaji wake  chipukizi  kwa  kuonyesha  ari  na  ujasiri  katika  mchezo  dhidi ya  Sweden.

Mwandishi : Sekione  Kitojo / dpae/rtre /afpe

Mhariri : Sudi  Mnette