Udondozi wa magazeti
26 Agosti 2010Tunafungua sasa kurasa za magazeti ya Ujerumani ambapo wahariri wa leo wametuwama zaidi katika suala la ulinzi wa data za wafanyakazi, kusitishwa kwa sheria ya kuwaandikisha vijana kutumikia jeshi kwa mujibu wa sheria na pia madai ya kutaka waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani , Guido Westerwelle kujiuzulu.
Tukianza na gazeti la Frankfurter Rundschau, linaandika kuhusu ulinzi wa data za wafanyakazi, katika mahali pa kazi.
Gazeti linaandika kuwa muswada wa sheria hiyo pia hauko timilifu , ili kuweza kushughulikia suala la kuwalinda wafanyakazi dhidi ya waajiri wao ambao ni wadadisi. Hii inahusiana na kupigwa marufuku uwekaji wa kamera katika maeneo ya kazi. Waajiri wanalipinga suala hilo la kupigwa marufuku, kwa msingi kuwa linazuwia kuwadhibiti wale wafanyakazi ambao ni wadokozi.
Gazeti la Abendzeitung la mjini Munich , kuhusiana na mada hiyo linaandika.
Kwa wafanyakazi wa kuajiriwa wanaweza kuwa katika hali ya kudhalilishwa, anasema makamu wa mkuu wa kundi la wabunge wa vyama vya CDU na CSU katika bunge la Ujerumani , Michael Fuchs. Haiwezekani , kwamba wafanyakazi wanacheza tu katika mtandao wa internet kutwa nzima. Hapa anashauri Fuchs haiwezekani mfanyakazi kuwa amepata mafunzo, na wakati huo huo akawa hana ujuzi wa kutosha. Kwa hali yoyote iwayo muajiri ni lazima amlinde dhidi ya uhalifu.
Nalo gazeti la Westfälische Nachrichten öa mjini Münster , linazungumzia mada hiyo hiyo.
Serikali ya Ujerumani ni wazi imelazimishwa kuingia katika mjadala huu. Baada ya kashfa ya ulinzi wa data katika makampuni ya kuuza biadhaa ya Lidl, kampuni la simu , Telecom na shirika la reli , Deutsche Bahn, serikali hatimaye imeweza kutoa rasimu ya sheria, na kuweka mipaka ya uchunguzi wa wafanyakazi. Sheria hiyo ambayo imeidhinishwa tayari na baraza la mawaziri, anaiangalia mhariri kuwa ni ya dunia asiyoifahamu. Anasema mhariri, kwa hiyo si muhimu basi kupiga marufuku uchukuaji wa data kutoka katika mitandao ya kijamii katika internet?
Mada nyingine iliyoandikwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani , inahusu kusitishwa kwa sheria ya kuwaandikisha vijana jeshini kwa mujibu wa sheria. Gazeti la die tagespost la mjini Würzburg linaandika.
Ikiwa jeshi la Ujerumani Bundeswehr likiundwa hivi karibuni na wanajeshi wa kuajiriwa na wale wa muda, au wa kujitolea basi hilo litakuwa jeshi la kampuni ya ulinzi. Iwapo jeshi hilo litapoteza uhusiano na jamii ya Ujerumani , kwa kuwafanya watu wa taifa hili kutotumikia jeshi hilo kwa mujibu wa sheria, basi itavunja moja kati ya mhimili mkuu ambao pia uko katika katiba ya nchi hii. Na iwapo jengo hilo litavunjika, basi itakuwa imeundwa nafasi mpya ya matamanio yasiyoweza kudhibitiwa ya uzalendo na hali ya kutovumilia hali ambayo jamii yetu haihitaji.
Gazeti la der neue tag linaandika kuhusu madai ya kutaka waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani ajiuzulu. Gazeti linaandika.
Paka akitoka panya hutawala. Guido Westerwelle anafahamu hilo. Lakini pamoja na kufahamu hilo, wakati wote Westerwelle amekuwa akijishughulisha tu na mambo ya kigeni. Kwa hiyo wakati akiwa katika ziara yake hivi sasa ya mataifa ya eneo la Balkan , huku nyuma kuna wito unaotolewa kutaka ajiuzulu. Viongozi wenzake wanashindwa kumkingia kifua. Shutuma za Rainer Brüderle kutokana na matokeo mabaya ya uchaguzi uliopita ni hatari kwake. Kutokana na uchunguzi wa maoni ya wapiga kura kuwa chini , anapaswa kufanyia kazi hilo ili kubadili hali hiyo katika chama chake.
Mwandishi : Sekione Kitojo / Inlandspresse
Mhariri : Mwadzaya,Thelma