1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UDONDOZI WA MAGAZETI

Erasto Mbwana6 Septemba 2005

Maoni ya Wahariri wa magazeti ya Ujerumani yaliyotoka leo asubuhi yamejishughulisha na misaada ya kuwasaidia Wahanga wa gharika ya Katrina nchini Marekani; Uchaguzi mkuu wa Ujerumani na upunguzaji wa Wafanyakazi katika kampuni ya kutengeneza magari ya Volkswagen.

https://p.dw.com/p/CHMt

Gazeti la “FRANKFURTER ALLGEMEINE” likijishughulisha na misaada ya serikali ya Marekani ya kuwasaidia Wahanga wa gharika ya Katrina limeandika:

“Taifa halikujitayarisha vya kutosha au la sivyo isingalichukua siku tano hadi sita kuwasaidia Wahanga wa balaa hilo. Kutokana na sera za ndani na nje za Marekani ambazo zimerekebishwa upya baada ya mashambulio ya kigaidi ya Septemba 11 lazima sasa watu wawajibike. Mtu wa kwanza anayepaswa kuwajibika ni Rais George W. Bush ambaye kwa aibu kubwa amekataa misaada ya kimataifa kwa masilahi ya kisiasa huku walala hoi elfu kadhaa wakipata taabu na kukosa huduma muhimu. Ni aibu kubwa kuona kuwa nchi kama Marekani haiwezi kuwasaidia haraka wananchi wake wenye shida.”

Hayo yalikuwa maoni ya “FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG.”

Gazeti la “RHEINISCHE POST” likijishughulisha na mada hiyo hiyo linakosoa kwa kuandika:

“Balaa hilo limefichua udhaifu wa Meya, Rais asiyejali maisha ya watu wake na wasaidizi ambao wamechoka kisaikolojia. Taifa lenye nguvu ulimwenguni limeonyesha utaahiri wake kusini mwa nchi hiyo. Lakini Marekani haionyeshi ukubwa katika udhaifu wake. Ni nchi duni na matunzo ya Nobel hutolewa wakati mbaya na mzuri. Inaanguka chini na baadaye husimama tena. Mtu ataweza kujionea hayo siku chache zijazo mjini New Orleans.”

Hayo yalikuwa maoni ya gazeti la “RHEINISCHE POST.”

Gazeti la “HANDELSBLATT” likijishughulisha na uchaguzi mkuu ujao nchini Ujerumani limeandika:

“Rais Kwasniewski wa Poland amesema kuwa uchaguzi mkuu wa Ujerumani ni miongoni mwa matukio muhimu kuhusu hatima ya Ulaya. Maoni haya ya mwanachama mpya wa Umoja wa Ulaya, Poland, kwetu sisi bado yangali mageni. Serikali mpya ya Ujerumani itakabiliwa na changamoto kubwa katika Umoja wa Ulaya na uwanja wa kimataifa baada ya Septemba 18. Changamoto hizo ni Katiba ya Umoja wa Ulaya, Iran na Mashariki ya Kati. Msimamo wa Ujerumani utatakiwa ujulikane kuhusu masuala hayo.”

Hayo yalikuwa maoni ya “HANDELSBLATT.”

Gazeti la “ABENDZEITUNG” likijishughulisha na mgombea ukansela wa vyama ndugu vya CDU/CSU, Bibi Angela Merkel, kukataa mdahalo wa pili wa Televisheni kati yake na Kansela Gerhard Schröder linauliza:

„Je, mgombea ukansela sasa ameingiwa na woga wa ghafla badala ya kuwa shujaa katika kutetea malengo yake? Siyo jambo zuri hata kidogo kwa Angela Merkel kukataa mpambano wa pili wa Televisheni na Kansela eti kwa sababu ana shughuli nyingi. Vyama vya CDU/CSU, kwa mujibu wa kura ya maoni, vinaongoza kiasi ambacho Bibi Merkel hana sababu hata kidogo ya kumwogopa Kansela Schröder.“

Hayo yalikuwa maoni ya gazeti la „ABENDZEITUNG.“

Gazeti la “KÖLNISCHE RUNDSCHAU” likitathmini upunguzaji wa Wafanyakazi katika kampuni ya kutengeneza magari ya Volkswagen limeandika:

„Uamuzi huo umechukuliwa majuma mawili kabla ya uchaguzi mkuu na hilo ni pigo kubwa kwa Kansela Schröder. Je, uamuzi huo una lengo la kukisaidia chama cha CDU katika uchaguzi mkuu? Hapana. Uamuzi uliotangazwa na Mkuu wa Kampuni ya VW Pischetsrieder wa kuwapunguza Wafanyakazi unatokana na matatizo yaliyopo. VW imekuwa chini katika mashindano ya kampuni zinazotengeneza magari kwa muda wa miaka mingi iliyopita. Kampuni za Kijapani, siyo peke yake, ambazo zinajipatia faida kubwa isipokuwa pia kampuni za Kifaransa za Renault na Peugeot/Citroén.“

Hayo yalikuwa maoni ya „KÖLNISCHE RUNDSCHAU.“

Gazeti la „MÄRKISCHE ODERZEITUNG“ nalo limeandika:

„Kampuni ya VW, tokea muda mrefu uliopita, ilikuwa katika ulimwengu mwingine kabisa. Wakuu wake wakiishi maisha ya anasa na fahari. Baraza la Wafanyakazi nalo, kutokana na ushawishi wake wa kisiasa, limethibitishiwa kisheria na kulipwa mishahara minono. Hayo yote yamekuwa yakiendelea hata bila ya kujali hali ya kiuchumi na muda wa kufanya kazi. Kusema kweli, kampuni hiyo imekuwa ikificha matatizo yake kwa muda wa miaka mingi. Kilichobakia sasa na hakuna njia nyingine hata kidogo ni kuchukua hatua kali na za dharura. Kupunguzwa Wafanyakazi ni afadhali kidogo kuliko kampuni yote ikiwa hatarini.“

Hayo yalikuwa maoni ya „MÄRKISCHE ODERZEITUNG.“

Gazeti la „KIELER NACHRICHTEN“ likijishughulisha na mada hiyo hiyo limeandika:

„Kampuni hii yenye makao yake makuu mjini Wolfsburg inakabiliwa na matatizo makubwa na ili iweze kuendelea lazima ichukue uamuzi. Inapaswa kutengeneza aina ya motokaa ambazo zitaziba pengo liliopo. Lakini jambo kama hilo halipo kwa wakati huu au iweze kutengeneza idadi ya motokaa zinazotakiwa. Hatua kama hiyo itasababisha Wafanyakazi wengi kupunguzwa. Uamuzi kama huo hautakuwa mgumu peke yake isipokuwa pia ghali. Kampuni ya VW lazima ibadilishe mifumo yake ya karne kadhaa zilizopita ya utawala, Baraza la Wafanyakazi na sera zake na iwe kama Kampuni ya kawaida ya kutengeneza magari.“

Kwa maoni hayo ya „KIELER NACHRICHTEN“ kuhusu kupunguzwa kwa Wafanyakazi wa kampuni ya kutengeneza magari ya Volkswagen ndiyo yote tuliyoweza kuwaletea kutoka magazeti ya Ujerumani yaliyotoka leo asubuhi.