1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchunguzi huru waanza Uingereza

24 Novemba 2009

Nchini Uingereza, uchunguzi uliyokuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu wa kushiriki wa nchi hiyo katika vita vya nchini Iraq unaanza leo, ambapo Waziri Mkuu wa zamani Tony Blair ni miongoni mwa watakahojiwa na tume maalum

https://p.dw.com/p/Ke8Q
Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Tony BlairPicha: AP

Katika vita hivyo vya Iraq, Tony Blair aliridhia kupelekwa kwa wanajeshi elfu 45 nchini Iraq kuuangusha utawala wa Saddam Hussein katika kile ambacho Marekani na washirika wake walisema ni kutafuta silaha za maagamizi ambazo walidai zikimiliwa na kiongozi huyo wa Iraq.

Ilikuwaje  Uingereza ikapeleka majeshi yake kuivamia nchi ambayo hakukuwa na ushahidi kuwa inamiliki silaha za maagamizi pamoja na kuwa na uhusiano na magaidi wa al Qaida?

Sir John Chilcot ambaye ni mwenyekiti wa tume hiyo, na mfanyakazi mstaafu wa serikalini, amewaonya mashahidi watakahojiwa na tume yake kutoficha lolote.

´´Tumejidhatiti kutoa taarifa kamili za uwazi na zisizo na upendeleo kutokana na ushahidi tutakaoupata´´

Sir Chilcot pia amesisitiza kuwa hakuna mtu ambaye atakuwa anashtakiwa na kwamba yeye na tume yake wanataka kuchunguza na kupata fundisho ya kile kilichotokea na si kuhoji.

Tume hiyo tayari imekwishakutana na baadhi ya familia za wanajeshi 179 wa Uingereza waliyouawa katika vita hivyo vya Iraq, ambapo walielezea wasi wasi wao kuwa iwapo majeshi hayo yalikuwa na silaha pamoja na mafunzo ya kutosha kuweza kukabiliana na adui, na pia kuezelea matumaini yao kwa tume hiyo.

Elysin Maning ni mama wa askari wa kike Staff Sergent Sharin Elliot aliyeuwa katika shambulizi la bomu la kutegwa pembezoni mwa barabara katika vita hivyo.

´´Tuna matumaini kuwa hatimaye ukweli utajulikana, na kwamba yuko atakayewajibika na kubeba lawama kwa yote yaliyotokea kwa watoto wote´´

Waziri Mkuu wa sasa wa Uingereza Gordon Brown ndiye atakayefungua pazia la kuanza kwa kazi za tume hiyo, pale atakapoelezea nini kilichotokea , na kuainisha funzo ambalo linaweza kupatikana kutokana na kushiriki kwa Uingereza katika vita hiyo.

Tony Blair  pamoja na wakuu wengine wa chama chake cha Labour atakuwa miongoni mwa wale watakahojiwa na tume hiyo, ingawaje huenda akaanza kutoa ushuhuda wake mwakani.

Mashahidi wa kwanza kufika mbele ya tume hiyo hii leo ni Peter Ricketts ambaye alikuwa  mwenyekiti wa kamati ya usalama kati ya mwaka 2000 na 2001 kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Mambo ya Nje kuwa afisa wa ngazi ya juu.

Wengine ni William Patey ambaye alikuwa mkuu wa idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Nje, Simon Webb aliyekuwa mkuu wa siasa katika Wizara ya Ulinzi, pamoja na Michael Wood aliyekuwa mshauri wa sheria katika Wizara ya Nje.

Mnamo siku za nyuma kumefanyika uchunguzi rasmi mara mbili, kuhusiana na mazingira yaliyosababisha azma ya kushiriki kwa majeshi ya Uingereza katika uvamizi huo nchini Iraq,lakini baraza la mawaziri lilikataa kuwepo kwa uchunguzi kamili mpaka kwanza hatua ya kuyapeleka majeshi hayo ikamilike.

Hata hivyo kabla ya kuanza kazi kwa tume hiyo kumekuwa na shutuma kuwa, tume hiyo haina uwezo wa kushughulikia suala muhimu, kama iwapo hatua ya uvamizi huo  ilikuwa halali kisheria, kwani katika kamati hiyo hakuna wanasheria na majaji.

Mwandishi.Aboubakary Liongo/AP/BBC

Mhariri:Mohamed Abdul-Rahman