1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchumi wa Zimbabwe wazidi kuboromoka.

Mohammed Abdul-Rahman11 Julai 2007

Ripoti zinasema kuna mpango wa kuifungamanisha sarafu ya Zimbabwe -dola na rand ya Afrika kusini, lakini zinakanushwa na serikali mjini Harare.

https://p.dw.com/p/CHB8
Rais mkongwe barani Afrika , Robert Mugabe wa Zimbabwe.
Rais mkongwe barani Afrika , Robert Mugabe wa Zimbabwe.Picha: dpa

Serikali ya Zimbabwe imekanusha kwamba inazingatia uwezekano wa kuifungamanisha sarafu yake ya dola na ile ya rand ya Afrika kusini, kama sehemu ya mpango wa kuitoa nchi hiyo katika hali mbaya ya kiuchumi inayoikabili.

Gavana wa benki kuu ya Zimbabwe Gideon Gono amesisitiza kwamba wazo la kuifungamanisha sarafu ya Zimbabwe na ile ya Afrika kusini halikuzungumzwa.Matamshio yake yamekuja wakati kukiwa na ripoti kwamba maafisa wa Jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika SADC walikua na mazungumzo juu ya uwezekano huo.

Wakati vyombo vya habari vya serikali ya Zimbabwe vilithibitisha kwamba Katibu mtendaji wa jumuiya ya SADC Tomaz Salomao na baadhi ya maafisa wake walikuweko mji mkuu wa Zimbabwe Harare juma lililopita, viliitaja ziara hiyo kuwa ya kawaida tu.

Bw Salomao alipewa jukumu na mkutano wa viongozi wa jumuiya hiyo mwezi Machi, kutathimini njia zitakazoweza kuikwamua Zimbabwe kutokana na hali yake mbaya ya kiuchumi, ambapo ughali wa maisha sasa unatajwa kufikia zaidi ya asili mia 5,000.

Ripoti ya gazeti la Sunday Independent la Afrika kusini hivi majuzi, ilisema kwamba mazungumzo mjini Harare mazungumzo yamekua yakifanyika kujadili juu ya uwezekano wa kuiingiza Zimbabwe katika mfumo wa matumizi ya fedha wa pamoja unaozijumuisha Afrika kusini, Namibia, Lesotho na Swaziland.

Akiulizwa juu ya ripoti hiyo katika mkutano na waandishi habari mjini Pretoria jana, Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Afrika kusini Bibi Nkosozana Dlamini Zuma alikataa kuzungumzia suala hilo moja kwa moja, ingawa alikiri kwamba serikali yake ina wasi wasi na hali mbaya ya uchumi wa jirani yake upande wa kaskazini akimaanisha Zimbabwe.

Hali hiyo ilianza kuwa mbaya zaidi wiki mbili zilizopita, baada ya Rais Robert Mugabe kuamuru bei za bidhaa zote zipunguzwe kwa asili mia 50. Polisi wakawatia nguvuni wafanya biashara waliokataa kutii amri hiyo.

Afrika kusini inahofia endapo hali itazidi kuwa mbaya, itasababisha wimbi zaidi la wakimbizi kutoka Zimbabwe. Tayari hivi sasa kuna zaidi ya Wazimbabwe milioni 3 walioingia Afrika kusini kinyume cha sheria wakikimbia hali ngumu ya maisha nchi mwao.

Akizungumza mjini Johannesburg Askofu wa kikatoliki wa jiji la Bulawayo nchini Zimbabwe Pius Ncube ambaye ni mkosoaji mkubwa wa utawala wa Rais Mugabe, alimtaka kiongozi huyo sasa astaafu. Akaongeza kwa kusema “Mugabe ni mtu anayependa madaraka na anaishi kwa ajili ya madaraka. Huyu ni mtu wa miaka 83 na atakaposimama tena kwenye uchaguzi mwakani atakua 84. Hata chama chake ZaNU-PF kinamuomba, tafadhali n´gatuka umefanya mazuri ya kutosha….. bila shaka kwa mtazamo wa ZANU-PF, lakini kwa mtazamo wangu mimi amefanya maovu mengi.”