1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Rashia na Iran Magazetini

5 Machi 2012

Uchaguzi wa rais na matokeo yake nchini Rashia,Uchaguzi wa bunge nchini Iran na mpango wa kumsusia mgombea wa kiti cha rais nchini Ufaransa Francois Hollande ni miongoni mwa mada zilizohanikiza magazetini.

https://p.dw.com/p/14F5n
Vladimir Putin ajitangaza mshindi wa uchaguzi wa raisPicha: picture alliance/landov

Tuanzie Rashia ambako wahariri takriban wote wa Ujerumani wanakubaliana uchaguzi wa rais uligubikwa na visa vya udanganyifu.Gazeti la "Badische Neueste Nachrichten" linaandika:Vladimir Putin anarejea Kremlin.Ameshinda uchaguzi wa rais,tangu duru ya kwanza.Hata hivyo ni ushindi "mchafu".Una kivuli cha hadaa na udanganyifu.Katika wiki zilizopita,wananchi wengi wa Rashia waliteremka majiani kudai uchaguzi wa kuaminika.Uchaguzi huu wa rais haukuwa wa kuaminika-kama ulivyokuwa uchaguzi wa Duma december mwaka jana.

Gazeti la "Südkurier" linashadidia hoja za udanganyifu na kuandika:Matokeo ya uchaguzi huo wa hadaa yalikuwa yakijulikana hata kabla ya vikaratasi vya kupiga kura havijajazwa:Rais mpya wa Rashia jina lake ni Vladimir Putin.Kurejea kwake Kremlin ni mbinu iliyoandaliwa miaka kadhaa iliyopita.Demokrasia ya hadaa ya Rashia hairuhusu njia nyengine.Suala linalozuka lakini ni Putin atafaulu kwa muda gani.Akrabu ya saa inazunguka kwa haraka.Mjini Moscow na St.Petersburg kuna tabaka mpya ya wanaojiweza iliyoibuka.Hawataki pekee utulivu,wanadai pia haki ya kutoa maoni yao.Kiini macho hiki cha uchaguzi hawakubaliani nacho.Upinzani wao utakuwa mkali na hautasalia tena kichini chini.Kwa hivyo kishindo kikubwa kinamsubiri rais mpya wa Rashia.

Iran Wahlen Wahl 2012
Kiongozi mkuu wa kidini wa Iran Ayatollah KhameneiPicha: picture-alliance/landov

Uchaguzi wa bunge nchini Iran uliopelekea kambi ya kiongozi mkuu wa kidini Ayatollah Khamenei kuishinda kambi ya rais Mahmoud Ahmedinedjad ni mada nyengine iliyochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.Gazeti la "Neue Presse" linaandika:Ushindi wa wahafidhina katika uchaguzi wa bunge unabainisha kwamba madaraka ya Ayatollah hayajatetereka hata kidogo.Kwa nchi za magharibi hizo si habari nzuri.Ingawa Ahmadinedjad anaangaliwa kama "mchokozi" hata hivyo katika mvutano kuhusu mradi wa kinuklea wa Iran,mara nyingi amekuwa akijaribu kuonyesha ishara za kutaka maridhiano.Mara nyingi amekuwa akikaripiwa na Khamenei.Mteule wake Laridjani,ingawa anatajikana kuwa mtu mwenye hikma,lakini anafuata msimamo mkali zaidi kuliko Ahmadinedjad na kamwe hatoyawekea suala la kuuliza madaraka makubwa aliyo nayo Ayatollah.

Frankreich Wahlkampf Sarkozy Merkel Monti
Kansela Angela Merkel(kulia) ,rais Sarkozy wa Ufaransa na waziri mkuu wa Italy Mario Monti (kushoto)Picha: dapd

Ripoti yetu ya mwisho magazetini inahusu dhana za kuwepo mpango wa kumsusia mgombea wa kiti cha rais kutoka chama cha kiisoshialisti cha Ufaransa Francois Hollande.Gazeti la "Frankfurter Rundschau" linaandika:Kwakua Francois Hollande anashuku mpango wa kuleta utulivu wa sarafu ya Euro-hiyo ingebidi iwe sababu ya watu kuzungumza nae.Wangejaribu kumtanabahisha kwamba njia anayofuata siyo.Kwasababu kila kitu kinaonyesha kwamba mwezi ujao, wafaransa watamchagua bwana huyu huyu awe rais wao.Kwa namna hiyo hata viongozi wa taifa na serikali wa kutoka vyama vya kihafidhina watalazimika sio tu kuzungumza nae,watamhitaji kuweza kusonga mbele katika masuala ya Ulaya.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Abdul-Rahman Mohammed