1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Rais nchini Ufaransa kesho.

Mohammed Abdul-Rahman20 Aprili 2007

Kampeni yamalizika jana (ijumaa) usiku, huku wagombea wakitoa rai ya mwisho kwa wapiga kura.

https://p.dw.com/p/CHFl
Bw Bayrou na Bibi Royal (kulia). Inaashiriwa mmoja wao atachuana duru ya pili na mgombea wa chama tawala Bw Sarkozy tarehe 6 mwezi ujao.
Bw Bayrou na Bibi Royal (kulia). Inaashiriwa mmoja wao atachuana duru ya pili na mgombea wa chama tawala Bw Sarkozy tarehe 6 mwezi ujao.Picha: AP Graphics/DW

Kampeni ya uchaguzi wa Rais nchini Ufaransa imemalizika jana usiku tayari kwa wapiga kura kuamua hapo kesho katika duru ya kwanza ya uchaguzi huo , katika kile kinachosubiriwa kuwa kizazi kipya cha uongozi mkuu nchini Ufaransa.

Kuna jumla ya wagombea 12 katika uchaguzi huo wa kesho Jumapili itakayokua duru ya kwanza kabla ya wagombea wawili wa usoni kuchuana kwa duru ya mwisho tarehe 6 mwezi ujao.

Kwa mujibu wa utafiti wa maoni ya wapiga kura, waziri wa zamani wa mambo ya ndani kutoka chama cha mrengo wa kulia UMP, Nicolas Sarkozy anaongoza, mgombea wa chama cha Kisoshalisti Bibi Segolene Royal ameonekana kuziba pengo hilo katika siku za karibuni, akifuatwa na Francois Bayrou kutoka chama cha UDF cha siasa za kati- hali ambayo inayafanya matokeo kuwa magumu kutabiri.

Lakini mgombea aliyezusha mshangao kwa wengi 2002, kiongozi wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia Front National Jean Marie Le Pen , alipomaliza wa pili duru ya kwanza na hatimae kuchuana na Rais Jacques Chirac katika duru ya pili , licha ya kutoa bado changamoto haielekei kama atafanikiwa tena safari hii.

Chirac kutoka enzi ya wanasiasa waliotokana na Jenerali Charles de Gaulle baada ya vita vya pili vya dunia, kizazi kinachoonekana hatimae ku´ngatuka, anastaafu baada ya kuiongoza Ufaransa kwa miaka 12, na wagombea wa safari hii-wote wamo kwenye maika ya 50 isipokua Le Pen anayetokana na kizazi cha kina Chirac.

Utafiti wa maoni ya wapiga kura hadi jana umeashiria Sarkozy akiongoza duru ya kwanza kwa asili mia kati ya 27 na 29 ya kura, Royal kati ya 22 na 25 ya kura, Bayrou kati ya 15 na 20 asili mia na Le Pen kati ya 13 na 15.

Wadadisi wanasema ikiwa duru ya pili itakua kati ya Sarkozy na Royal basi Sarkozy ataibuka mshindi kwa kura kati ya asili mia 50 na 53 dhidi ya asili mia kati ya 47 na 50.

Lakini Bayrou atakua na nafasi nzuri ya kumshinda Sarkozy pindi akiingia duru ya pili. Bayrou amekua kivutio kutokana na siasa zake za wastani, wakjati Sarkozy anamkosolewa kwa msimamo wake kuhusu wahamiaji ikitajwa pia kwamba anaitumia hali hiyo kuwavutia wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia.

Kwa upande Bibi Royal aliyewaangusha vigogo ndani ya chama chake cha Kisoshalisti kushinda nafasi ya kuwa mgombea, huenda akakabiliwa na changa moto kubwa kutokana na ile dhana ya kwamba bado Ufaransa haiko tayari kumvumilia mwanamke kuwa Kiongozi wa taifa hilo. Lakini wakati wengine wanasema hicho si kiegezo, uchaguzi huu wa rais nchini Ufaransa ulioshuhudia uadikishaji mkubwa kabisa wa wapiga kura, unazusha shauku kubwa ndani na nje ya Ufaransa yenyewe.