1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa rais nchini Mali Jumapili

Mohammed Abdul-Rahman27 Aprili 2007

Rais wa sasa Toumani Toure aekewa matumaini ya kushinda.

https://p.dw.com/p/CHFJ
Rais wa Mali Amadou Toumani Toure
Rais wa Mali Amadou Toumani TourePicha: AP

Wapiga kura nchini Mali kesho wataelekea kwenye vituo vya kuzpigia kura katika uchaguzi wa Rais, ikiwa ni hatua nyengine ya kuimarisha mkondo wa demokrasia nchini humo ulioanza 1991. Rais wa sasa Amadou Toumani Toure anagombea tena kipindi kingine cha miaka mitano akiwa mgombea wa kujitegemea, lakini anaungwa mkono na muungano wa vyama viwili vikubwa pamoja na mlolongo wa vyama vidogo vidogo.

Jenerali huyo wa zamani aliyaongoza mapinduzi yalimuangusha dikteta Mousa Taraoure 1991 na kuanzisha mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, kabla ya kukabidhi madaraka kwa raia. Baada ya kustaafu jeshini akajikita katika siasa ana kugombea uchaguzi wa rais mwaka 2002, ulipomalizika muda wa aliyekua rais wakati huo Alpha Oumar Konare ambaye sasa ni rais wa halmashauri kuu ya umoja wa Afrika.

Wapinzani wakubwa wa Toure katika uchaguzi wa kesho, ni kiongozi maarufu wa upinzani Ibrahim Boubacar Keita, aliyewahi kuwa waziri mkuu na spika wa bunge la taifa.

Keita aliyemaliza nafasi ya tatu katika uchaguzi wa 2002, ni sehemu ya muungano wenye wagombea wengine watatu katika uchaguzi huo.

Wanasiasa hao wamesaini amakubaliano kuhusu duru ya pili, kwamba watamuunga mkono yeyote atakayeingia duru ya pili miongoni mwao, lakini wachambuzi wanasema tayari hali hiyo inaweza kumpa mwanya Toure kushinda moja kwa moja katika duru ya kwanza.

Mhadhiri wa siasa na saikolojia katika chuo kikuu cha Bamako Profesa Mamadou Samake, anasema kwamba ingawa hakuna taasisi ya utafiti wa maoni ya wapiga kura, lakini Rais Toure anaelekea kuwa na nafasi kubwa ya kushinda, kutokana na namna alivyotokeza na kuripotiwa katika vyombo vya habari pamoja na ziara zake nyingi za kampeni katika maeneo ya ndani nchini humo, licha ya kukosolewa na wapinzani kuhusika na sera zake za kiuchumi.

Mali , nchi isiyo na bandari imeathirika kutokana na mzozo nchini Ivory Coast ambayo ni nchi jirani muhimu kwa bidhaa zinazoingia Mali. Sambamba na hayo imekumbwa na matatizo ya ukame na uvamizi wa nzege ulioathiri mapato ya 70 asili mia ya wakaazi wa maeneo ya mashambani.

Hata hivyo akijibu shutuma za wapinzani wake, Kiongozi huyo ambaye kampeni yake imegharimiwa vizuri zaidi kuliko wapinzani wake, amekua akitembelea maeneo mbali mbali, na kugusia juu ya miradi mbali mbali aliyoianzisha ikiwemo ya kilimo , miundo mbinu, afya na ujenzi. Pia hivi karibuni alipata uungaji mkono wa waasi wa zamani wa Touareg waliosaini mkataba wa amani na serikali baada ya mpigano mwezi Mei , 2006.

Sambamba na hayo, Rais Toure ana uhusiano mzuri na Ufaransa, Libya na Marekani na Marekani iliimarisha ushirikiano wake hivi karibu na Mali, katika sekta ya afya,elimu na kile inachokiita vita dhidi ya ugaidi.

Mwana diplomasia mmoja akiusifu uongozi wa Rais Toumani Toure anasema, serikali yake haina kashfa ya fedha wala rushwa. Kiongozi huyo amejiweka kuwa mtu wa kawaida na kuna uhuru mkubwa wa vyombo vya habari. Baada ya uchaguzi wa rais hapo kesho, uchaguzi wa bunge utafanyika mwezi Julai.