1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Mchujo : Jumanne Kabambe Marekani

1 Machi 2016

Leo ni "Super Tuesday" au Jumanne Kabambe siku muhimu katika kinyanganyiro cha kuwania urais wa Marekani ambapo uchaguzi wa mchujo unafanyika katika majimbo 12 ikiwa ni pamoja na majimbo yenye idadi kubwa ya watu.

https://p.dw.com/p/1I4hg
Wagombea wanowekewa matumaini Hilary Clinton wa chama cha Demokratik na Donald Trump wa Republikan.
Wagombea wanowekewa matumaini Hilary Clinton wa chama cha Demokratik na Donald Trump wa Republikan.Picha: Getty Images/J.Raedle/picture-alliance/dpa/D.Van Tine

Wajumbe wengi watapiga kura kuchaguwa wagombea watakaowakilisha vyama vyao katika uchaguzi mkuu wa Marekani baadae mwaka huu.Mgombea anayewekewa matumaini kukiwakalisha chama cha Demokratik ni Hilary Clinton wakati chama Republikan mashaka yanazidi kuongezeka iwapo itawezekana kumzuwia Donald Trump asikiwakilishe chama hicho.

Takriban kama theluthi moja ya kura za wajumbe wa chama cha Repbulikan zitapigwa leo hii kwa chama cha Demokratik ni kama asilimia ishirini hivi.Na kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni wa hivi karibuni kabisa hofu imezagaa miongoni mwa vigogo wa chama cha Republikan.

Donald Trump ana nafasi nzuri ya kushinda majimbo yote isipokuwa Texas.Kila mwanachama wa Republikan anaona sasa Trump hazuiliki tena.

Juu ya kwamba bilionea huyo hakuonyesha chochote cha uungwana hadi sasa.Trump alimdhihaki mpinzani wake mkuu seneta wa Florida Marco Rubio katika kampeni zinazoendelea za mchujo kwa kumpachika majina mbali mbali.

Trump amesema "Marco Rubio mdogo,mdogo kabisa uzito wake wa ni featherweight haufikii hata ule uzito wa kiwango chepesi."

Rubio atapatapa

Marco Rubio ni mtu muhimu kuzuwiya mlolongo wa ushindi wa Trump.Iwapo atashinda hapo tarehe 15 mwezi wa Machi katika jimbo lake la Florida kama anavyotaraji hapo Trump anaweza kudhibitiwa.

Seneta Marco Rubio.
Seneta Marco Rubio.Picha: Reuters/N. Oxford

Lakini juhudi za seneta huyo za kumshinda Trump zinaonekana kutapatapa katika kampeni hiyo ya mchujo Rubio ameuliza Je mmeiona mikono ya Trump.Ni midogo mno na mnajuwa watu wanavyosema kuhusu wanaume wenye mikono midogo .......

Hata Warepulikan wana wakati mgumu kuchuana na Trump limeandika gazeti la Washington Post.Trump amewahamasisha wapiga kura wa sera kali za mrengo wa kulia na wale ambao zamani walikuwa wa chama cha Demokratik wafanyakazi, wazungu wasiokuwa na shahada ya chuo kikuu,watu walioko tabaka la kati wanaojiona kuwa hatarini. Trump anawapa moyo kwamba ni mikono madhubuti tu ndio itakayoweza kuiongoza Marekani.

Marekani haikuwahi kusita kuwa adhimu

Hilary Clinton wa chama cha Demokratik ndie anayewekewa matumaini ya kushinda leo hii katika uchaguzi wa mchujo wa Super Tuesday,hususan katika majimbo ya kusini yenye Wamarekani weusi wengi na Wamarekani wenye asili ya Amerika kusini mpinzani wake Bernie Sanders ana nafasi ndogo. Kampeni za Clinton za karibuni zilimlenga zaidi Trump

Ramani ya majimbo ya uchaguzi Marekani 2016.
Ramani ya majimbo ya uchaguzi Marekani 2016.

Clinton amesema "Marekani katu haikuwahi kuacha kuwa adhimu.Hakuna haja kwa Marekani kuwa adhimu tena. Kwa sababu Marekani katu haikusita kuwa adhimu."

Badala ya kujenga kuta kama alivyopendekeza Trump na kuigawa nchi Clinton ametaka Marekani iwe kitu kimoja tena.

Hata hivyo Bernie Sanders anataraji kufanya vizuri katika jimbo lake la Vermont na katika jimbo jirani la Masachussets. Wengi wanazungumzia zaidi juu mpambano wa Noemba nane kati ya Clinton na Trump.

Mwandishi : Ganslmeier, Martin / Mohamed Dahman

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman