Uchaguzi nchini Msumbiji
28 Oktoba 2009Rais Armando Guebuza alikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kupiga kura leo, akitumbukiza kura yake saa moja baada ya vituo vilipofunguliwa saa 12 za asubuhi. Chama tawala cha Frelimo kinachuana na chama cha Ki-Conservative cha Renamo, na vyama hivyo viwili vilipigana vita vya kienyeji vilivodumu miaka 16 baina yao kati ya mwaka 1976 na 1992. Renamo ilikuwa inasaidiwa na serikali ya kibaguzi ya Afrika Kusini ya wakati huo pamoja na Rhodesia ambayo sasa ni Zimbabwe.
Watu milioni 10.3 wana haki ya kupiga kura hii leo kwa ajili ya uchaguzi wa urais na wa bunge la wajumbe 250. Licha ya hayo, mabunge mepya ya mikoa 10 yanachaguliwa wakati huo huo. Mpiga kura Vasco Munguambe ambaye amekuwa leo asubuhi akingojea kupiga kura, alisema: " ni muhimu kupiga kura kwa vile mustakbali wa nchi unaamuliwa; nataka kutoa maoni yangu juu ya vipi hali ya baadae ya nchi iwe."
Katika miaka michache iliopita, Msumbiji yenye wakaazi milioni 20, moja wapo ya nchi maskini kabisa duniani, imekuwa moja wapo ya nchi inayosifika sana barani Afrika kwamba imepata mafanikio. Uwekezaji mkubwa wa kutoka ng'ambo katika sekta za gesi ya ardhini, makaa, umeme wa kutoka nguvu za maji, madini pamoja na nyinginezo zimeufanya uchumi wa nchi hiyo kupanda, na ukuuaji huo unatarajiwa kufikia asilimia tano mwaka huu.
Armando Guebuza, mfanya biashara aliye tajiri, anatazamiwa kwa urahisi kushinda kwenye uchaguzi huu na kuwa rais kwa kipindi cha pili. Katika mkutano wa hadhara wa kampeni yake, rais Gebuta alisema:
" Chama cha Frelimo kitafanya kile ambacho maisha kimefanya nchini msumbiji. Hakika ushindi ni wetu."
Na kwa nafasi ya pili, kiongozi wa Renamo, Alfondo Dlakama, anakabiliana na ushindani mkali kutoka kiongozi wa chama kipya, Daviz Simango, ambaye ni meya wa mji wa Beira ulioko katikati ya nchi hiyo. Yeye alikiacha chama cha Renamo mwaka jana baada ya kutokea kutofahamiana ndani ya chama hicho, na akaamua kuunda chama cha Democratic Movement, MDM. Amekuwa na miezi sita kutayarisha kampeni ya uchaguzi ya chama chake kipya. Chama hicho, ambacho kimezusha hamu miongoni mwa wapiga kura vijana, kimezuiliwa na tume ya uchaguzi, ilio na wanachama wa Frelimo na Renamo, kushindania baadhi ya wilaya za uchaguzi kwa ajili ya uchaguzi wa bunge. Kwa ujumla, vyama 19 vinashindana katika uchaguzi huu, lakini ni Frelimo na Renamo tu vilivokubaliwa kuweka watetezi katika kila wilaya ya uchaguzi.
Ardio Evaristo, msemaji wa Chama cha MDM, alikuwa na haya ya kusema kabla ya siku ya leo ya uchaguzi:
"Demokrasia ya Msumbiji iko katika hali mbaya. Vyama vya zamani vya Frelimo na Renamo maisha vimefikiri vimeiletea Msumbiji demokrasia, lakini vyama hivyo havitendi kwa njia ya kidemokrasia. Vinawadharau wananchi na vinafanya kama vile vinaimiliki nchi nzima. Hakuna demokrasia ya kweli, wanalitumia tu midomoni neno demokrasia ili kuwaweka gizani sehemu ya wananchi."
Matokeo ya mwanzo kutoka vituo 12,000 vya kupigia kura yanatarajiwa kuanza kumiminika baada ya vituo hivyo kufungwa jioni ya leo, lakini ni Novemba 2 ambapo matokeo ya mwisho yatatangazwa.
Mwandishi: Othman Miraji /AFP
Mhariri:M.Abdul-Rahman