1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi Cote D'Ivoire.

9 Desemba 2010

Shinikizo zaidi zatolewa kwa Laurent Gbabo.

https://p.dw.com/p/QUXM
Laurent Gbagbo,akiapishwa katika ikulu kama rais wa Cote D'Ivoire.Picha: AP

Afrika kusini na Kenya zimejiunga na Umoja wa Mataifa kumuomba kiongozi aliyeshindwa katika uchaguzi uliokumbwa na mzozo nchini Cote d´Ivoire Laurent Gbabo ,akubali kushindwa na kuacha  kung'ang'ania uongozi .

Waziri mkuu wa Kenya Raila Odinga amemtaka Laurent Gbabo kukubali kushindwa na ameiomba jumuiya ya kimataifa kumlaumu kwa vurugu zilizofanyika nchini  Cote D'Ivoire tangu kufanyika awamu ya pili ya uchaguzi tarehe 28 mwezi uliopita wa Novemba.

Akizungumza kando ya mkutano wa tabia nchi  unaofanyika mjini Cancun Mexico,Raila amesema Cote D'Ivoire inakabiliwa na janga ambalo bara la Afrika haliwezi kulihimili.

Afrika kusini ambayo ndio nchi yenye uchumi mkubwa barani Afrika imemtaka Gbagbo kuheshimu na kutii makubaliano yaliotolewa na muungano wa Afrika na jumuiya ya kiuchumi ya mataifa 15 magharibi mwa Afrika - ECOWAS, yaliosema kwamba ataondoka madarakani.

Baraza la usalama la Umoja wa mataifa hapo jana lilisema kwamba linamuunga mkono Alassane Ouattara, na hii imedhibitisha kuungwa mkono kiongozi huyo mpya kimataifa.

Katika taarifa yake, baraza hilo hilo limesema kwamba linashutumu vikali jitihada zozote za kukiuka mapendeleo ya wananchi au kudharau uadilifu wa mpango mzima wa uchaguzi  au uchaguzi huru na wa haki uliofanyika nchini humo.

Taarifa hiyo imeendelea kusema kwamba baraza hilo la usalama litaidhinisha hatua zilizolengwa dhidi ya wale watakaojaribu kuharibu mpango wa kutafuta amani nchini humo au watakao kiuka kwa ukubwa haki za binaadamu na sheria ya kimataifa ya kibinaaadamu.

Taarifa hii ya baraza la usalama ilitolewa baada ya mjumbe wake maalum nchini Cote D'Ivoire YJ Choi kuliarifu kwamba Outtara alishinda uchaguzi huo wa Novemba tarehe 28 kwa tofauti isiyoweza kupingika dhidi ya Gbabo.

Elfenbeinküste Unruhen Dezember 2010
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Cote D'Ivoire, Choi Young-jin.Picha: AP

Laurent Gbabo anayelidhibiti kwa jina tu, jeshi nchini humo, na kituo cha televisheni ya taifa, hajaonyesha ishara zozote za kuachilia uongozi wake wa miaka 10 wa nchi hiyo iliyo na utajiri wa Cocoa, na ametangaza serikali yake hapo jana.

Kwa upande wake Ouattara ametangaza pia serikali pinzani,  na waziri wake mkuu Guillaume Soros  amesema wameanza kuwabadilisha mabalozi wake katika nchi kuu na kuchukua hatua za kudhibiti fedha za umma.

Kwa mujibu wa shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu, Amnesty International, vurugu za uchaguzi huo zimesababisha kufariki kwa watu takriban 20.

Wachambuzi wanasema viongozi hao wawili huenda wakalazimika kujadili makubaliano ya kugawana mamlaka, lakini kiongozi mkuu wa ECOWAS rais wa Nigeria Goodluck Jonathan  amelipinga hilo akisema kwamba suala hilo halijafanikiwa vizuri nchini Kenya na Zimbabwe.

Mwandishi: Maryam Abdalla/AFPE/DPAE

Mhariri: Abdulrahman.