1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uamuzi wa kupunguza ruzuku ya kilimo waharibu masoko ya Afrika

Josephat Nyiro Charo21 Novemba 2008

Mawaziri wa kilimo wa Umoja wa Ulaya wataka kupunguza ruzuku ya kilimo kwa wakulima

https://p.dw.com/p/FzGA

Mawaziri wa kilimo wa Umoja wa Ulaya wanataka kupunguza mabilioni ya ruzuku inayotolewa kila mwaka kwa ajili ya kilimo na ufugaji. Hatua hii inaonekana kama mabadiliko madogo sana ikilinganishwa na matumaini makubwa yaliyopo kufanyika mageuzi ya sera za kilimo katika ngazi ya kimataifa.

Ng´ombe ni mnyama mwenye thamani kubwa kwa mfugaji. Nchini India ng´ombe ni kiumbe kitakatifu na huabudiwa kama mungu. Katika nchi nyingi barani Afrika ng´ombe huchukuliwa kuwa utajiri mkubwa na kitamaduni hutumiwa kulipia mahari. Barani Ulaya ukweli ni kwamba ng´ombe wana thamani kubwa kuliko mahali pengine popote dunaini. Mlipakodi katika Umoja wa Ulaya humlipia kila ng´ombe mmoja aliye shambani au zizini euro 2,5 kila siku. Watu bilioni 1,2 ulimwenguni hawana fedha kufikia kiwango hiki kwa ajili ya maisha yao ya kila siku na wanaishi katika hali ngumu ya kimaisha chini ya euro moja kwa siku.

Je mambo haya yana uhusiano gani? Fedha zinazolipwa hapa Ulaya kama ruzuku kwa wakulima na wafugaji hazimgharimu tu mlipa kodi wa Ulaya, bali pia zinayaharibu masoko ya kilimo barani Afrika. Kwa mkulima mwenye ng´ombe wanaotakiwa kulipiwa ruzuku, hawezi kuwa na mchungaji barani Afrika, hata kama anatakiwa kuwa na ng´ombe wa kisasa wanaotoa kiwango kikubwa cha maziwa na kuweza kupata chakula cha hali ya juu cha ng ´ombe wake walio zizini. Pamoja na hayo mkulima huyo hana ng´ombe wala uwezo wala chakula cha ng´ombe kinacholipiwa ruzuku. Hajawahi kumiliki zizi la ng´ombe ambamo angeweza kuwaweka ng´ombe wake.

Kama Wazungu, Wamarekani wanaunga mkono utandawazi na biashara huru. Katika mkutano uliojadili tatizo kubwa la kiuchumi duniani uliofanyika wiki iliyopita mjini Washington nchini Marekani, walitangaza msimamo huo wa pamoja. Mwaka wa 2005 pekee wakulima wa pamba nchini Marekani walilipwa ruzuku ya kiwango cha dola bilioni 4,2. Bila kujua hasa bei ya pamba, kwa kila tani moja ya pamba pengine fedha hizo zilikuwa nyingi mno kuliko kiwango kilichopatikana kutokana na mauzo ya tani moja ya pamba katika soko la kimataifa.

Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita wakulima 150,000 wamejiua nchini India. Wengi wao walikuwa wakulima wa pamba, wengi wanawake ambao hawakuweza tena kulipia mbegu, mbolea na dawa za kuulia wadudu zinazotengenezwa na kampuni kubwa za kimataifa kama Monsanto. Wengi wa wakulima hao walijiua kutumia mbolea. Hii huua kama sumu ya panya - polepole na kwa uchungu mkubwa.

Katika upande mwingine wa masoko ya kilimo ya Ulaya na Marekani, kodi kwa bidhaa zinazotoka nje ya masoko hayo zinaongezeka.Kwa njia hii watumiaji wa bidhaa hizi barani Ulaya na Marekani wanafungiwa kuweza kuzifikia bidhaa zenye thamani kutoka nchi zinazoendelea.

Ikiwa sasa uamuzi wa mawaziri wa kilimo wa Umoja wa Ulaya wa kufanya mabadiliko hayo madogo kuhusu kupunguza ruzuku ya kilimo ni jambo la kusheherekea, kimaadili hiyo ni kashfa kubwa. Kwa sababu uamuzi huo hautabidili mtizamo wa kimataifa kwamba ng´ombe mmoja katika Umoja wa Ulaya ana thamani mara mbili unusu zaidi kuliko maisha ya binadamu katika nchi zinazoendelea.