1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uamuzi kuhusu eneo la Abyei watolewa.

22 Julai 2009

Sudan ya Kaskazini na Kusini zimekubali uamuzi wa mahakama ya kudumu ya upatanishi ya The Hague

https://p.dw.com/p/IvNQ
Makamu wa rais wa Sudan, Silva Kiir (kushoto) na rais wa Sudan Omar Hassan al BashirPicha: picture-alliance/dpa/dpaweb

Mahakama hiyo imehamisha mipaka ya eneo linalozozaniwa la Abyei nchini Sudan na kuifanya serikalia ya Sudan ichukuwe mamlaka ya maeneo hayo yaliyo na utajiri wa mafuta.

Wanajeshi zaidi wa Umoja wa Mataifa walikuwa wamepelekwa kabla ya kutolewa uamuzi huo wa leo juu ya hatima ya wilaya iliyo kati ya Sudan ya Kaskazi, eneo lililo na Waislamu wengi, na lile la Sudan ya Kusini lilinalokaliwa na Wakristo, kutokana na hofu kuwa huenda tena kungetokea mapigano kama yale ya mwezi Mei mwaka uliopita, na yaliosababisha vifo vya zaidi ya watu 100.

Mapigano hayo yaliyotokea katika mji wa Abyei pia yalisababisha maelfu ya watu kuyakimbia majumba yao na kutajwa kuwa ni kitisho kikubwa kwa makubaliano ya amani ya mwaka 2005 kati ya serikali ya Sudan na chama cha Sudan People`s Liberation Movement SPLM ambayo yalimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyo dumu miongo miwili . Hivyo vilikuwa vita vilivyodumu muda mrefu zaidi barani Afrika.

Huu ndio uamuzi wa mwisho na wa kisheria katia ya pande zote mbili, alisema naibu waziri wa masuala ya nje na afisa katika serikali ya Sudan. Viongozi wa eneo la Abyei walitazama kutolewa uamuzi huo kupitia runinga katika makao ya Umoja wa Mataifa .

Kundi la SPLM latoa tamko

Msemaji wa chama cha cha SPLM, Sudan People's Liberation Movement, Yahia Boulad, alisema kuwa uamuzi huo utaleta utulivu katika eneo hilo:alisema,

Kihistoria Abyei ni kati ya eneo la Sudan Kusini. Kuna mali asili nyingi katika eneo hilo, kama mafuta. Kwa kuligawa eneo la Abyei kwenda kusini au Kaskazini kutaleta utulivu katika eneo hilo na pia kulipa fedha eneo la Sudan Kusini.

Deng Alor, mpiganaji wa zamani kutoka Kusini mwa Sudan, ambaye sasa ni waziri wa mambo ya nje, alikuwepo wakati wa kutolewa kwa uamuzi huo, na alimsalimia waziri wa msuala ya ndani kutoka kaskazini mwa Sudan baada ya kutolewa uamuzi huo.

Sudan Aussenminister Deng Alor Kuol trifft Hosni Mubarak
Waziri wa mambo ya kigeni wa Sudan Deng Alor KuolPicha: AP

Alor alisema kuwa chama cha SPLM kitaukubali uamuzi huo wa mahakama, lakini akaongeza kuwa kuna haja ya kuuangalia zaidi uamuzi huo ili kubaini mahala maeneo ya vituo vya mafuta yalipo, baada ya afisa kutoka serikali ya Sudan kudai kuwa uamuzi ulilipa eneo la kaskazini vituo hivyo.

Kwa upande mwingine, Yahia pia alisema kuwa mipaka hiyo pia itatoa mwelekeo wa kura ya maoni hapo mwaka 2011 na kuongeza kuwa,

Wataelewa ni eneo gani liko kusini au kaskazini kwa kuwa hadi sasa hakuna mipaka. Na hii ni ishara ya mwaka 2011, ikiwa Sudan Kusini itapiga kura ya kuwa nchi huru.

Mjumbe maalumu wa Marekani nchini Sudan, Scott Gration, ambaye alikuwa amesafiri kwenda mji wa Abyei kabla ya kutolewa uamuzi huo, anasema kuwa ana matumaini kufuatia kutolewa kwa umuzi huo.

Gration alisema kuwa anaamini kuwa yale yaliyoafikiwa katika makubaliano ya pande hizo mbili yataafikiwa, na uamuzi wa mahakama ya upatanishi utatekelezwa.

Alisema kuwa Abyei ni eneo ambalo watu watafurahia manufaa yake ambayo yatakuja baadaye, pamoja na maendeleo yake.

Mwandishi :Jason Nyakundi/RTRE

Mhariri :Othman Miraji