Twiga: Mnyama aliye hatarini kuangamia
Kufuatia ujangili wa muda mrefu dhidi ya twiga na vifaru, hatari zinazokumba twiga zimeanza kudhihirika wazi. Idadi ya wanyama hao warefu kuliko wote duniani inazidi kupungua.
Maangamizi ya 'kimyakimya'
Idadi ya twiga imepungua katika miaka ya hivi karibuni huku wahifadhi wa wanyama wakionya kuhusu 'maangamizi ya kimyakimya' ya wanyama hao warefu zaidi duniani. Idadi jumla ya twiga walioko Afrika kusini mwa jangwa la Sahara ni 97,500 pekee. Huo ukiwa upungufu wa asilimia 40 tangu mwaka 1985. Hiyo ni kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Hifadhi ya Maumbile Asilia.
Wanyama wa 'pembe'
Wanyama hawa wanaovutia wameathirika kutokana na magonjwa, kupoteza mazingira yao na uwindaji haramu kwa ajili ya nyama yao, kando na kupata ajali za kugongwa na magari au nyaya za umeme. Kwa sasa kuna twiga wachache kuliko tembo barani Afrika. Wanaharakati wanasema twiga sasa wanakabiliwa na kitisho kingine kutoka kwa majangili wanaotoka Marekani kuelekea Afrika kutafuta pembe za wanyama.
Je kuna aina moja ya twiga– au nne?
Mnamo mwaka 2016, watafiti waligundua kuwa kuna aina nne tofauti za twiga wala si moja. Kwa sasa utafiti huo uliochapishwa kwenye jarida la Current Biology, unafanyiwa tathmini. Ikithibitika kuwa kuna aina nne za twiga, basi aina tatu zitakuwa katika kitisho cha kuangamia kulingana na orodha ya IUCN ya wanyama walioko katika hatari ya kuangamia, hali itakayohitaji juhudi zaidi za wahifadhi.
Ni vipi twiga walipata shingo ndefu?
Shingo za twiga zinaweza kuwa na urefu wa futi sita- licha kuwa zina nyuti za mgongo saba kama wanadamu, tofauti tu ni kwamba zao zimerefushwa. Ili damu ifike kwenye ubongo, lazima moyo uisukume kwa urefu wa mita mbili. Wanasayansi wangali wanajaribu kupata jibu la swali tata kuhusu ni vipi twiga walipata shingo ndefu.
Watoto hudondoshwa chini wanapozaliwa
Kipindi chao cha ujauzito ni kirefu, hudumu kwa miezi 15, na hukamilika kwa twiga kujifungua akiwa amesimama – ina maana kuwa mtoto hukaribishwa duniani kwa kuangushwa chini, urefu wa zaidi ya futi 5. Kwa kustahimili kishindo hicho, watoto wa twiga wanaelewa: wanaweza kusimama baada ya dakika 30 ya kuzaliwa na baada ya jumla ya saa 10 wakishazaliwa wanaweza kukimbia na mama zao.
Wanakula kila saa
Twiga hula kila wakati, hutafuna mamia ya tani za majani na matawi kila wiki na hutembea umbali mrefu kutafuta chakula. Lakini urefu wake hufanya unywaji maji kuwa ngumu na hatari. Wanalazimika kupanua miguu na kuinama, hali inayowaweka katika hatari ya kushambuliwa kiurahisi. Bahati nzuri ni kuwa wao hunywa maji mara moja tu baada ya siku kadhaa. Wanapata maji mengi kupitia majani wanayokula.
Kula huku akiburudika
Ulimi wa twiga wenye urefu wa inchi 21, ni kiungo muhimu kinachomsaidia kufikia majani ya juu ya miti– na pia humsaidia katika mchakato wa uzazi. Twiga hufikia majani na matunda ambayo wanyama wachache ndio huweza kufikia, huku akipenda sana mti aina ya acacia.