1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiAsia

Tsunami yaipiga Japan

Mohammed Khelef
1 Januari 2024

Nyumba zipatazo 33,500 hazina umeme katika eneo ambalo limepigwa na mfululizo wa matetemeko makubwa ya chini ya bahari nchini Japan, ambayo athari zake zimeshuhudiwa hadi kwenye miji ya mashariki ya mbali ya Urusi.

https://p.dw.com/p/4alIr
Onyo la tsunami kupitia simu za mkononi nchini Japan.
Onyo la tsunami kupitia simu za mkononi nchini Japan.Picha: Tosei Kisanuki/The Yomiuri Shimbu/AP/picture alliance

Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Japan lilisema tetemeko hilo la Jumatatu (Januari 1) lilikuwa na ukubwa wa 7.6 kwa kipimo cha Richter na miji iliyoathirika zaidi ni Toyama, Ishikawa na Niigata, yote kwenye kisiwa chake kikubwa cha Honshu katika mwambao wa magharibi wa Bahari ya Japan.

Shirika la habari la Urusi, TASS, limewanukuu mameya wa miji ya  Vladivostok na Nakhodka wakitangaza tahadhari ya tsunami katika maeneo hayo yaliyo kwenye kisiwa cha Sakhalin.

Soma zaidi: Japan yasema vipimo vya maji kulikotiririshwa maji ya Fukushima havionyeshi madhara

Onyo la mawimbi yenye ukubwa wa mita tatu lilitolewa pia kwenye baadhi ya maeneo ya Korea Kaskazini na Korea Kusini. 

Serikali mjini Seoul iliwataka wakaazi wa miji ya mwambao wa mashariki kuchukuwa hadhari ya kupanda kwa viwango vya bahari.

Watu watakiwa kuhama

Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Japan iliripoti matetemeko kwenye mwambao wa Ishikawa na maeneo yake ya karibu majira ya 10:00 jioni.

Mojawapo ya madhara ya tsunami iliyopiga eneo la Ishikawa nchini Japan.
Mojawapo ya madhara ya tsunami iliyopiga eneo la Ishikawa nchini Japan.Picha: Kyodo News/AP/dpa/picture alliance

Mamlaka hiyo ilitowa onyo la kutokea tsunami kubwa katika mwambao wa Ishikawa na matetemeko ya kiwango cha chini kwenye maeneo mengine katika mwambao wa kisiwa kikubwa cha Japan, Honshu.

Soma zaidi: Japan kuanza kutiririsha baharini maji ya kinu cha Fukushima

Televisheni ya shirika la utangazaji la Japan, NHK TV, iliripoti mawimbi yaliyofika ukubwa wa mita tano na kuwataka watu wa maeneo hayo kukimbilia milimani au kwenye mapaa ya majengo yaliyo karibu nao haraka iwezekenavyo.

Televisheni hiyo ilisema mawimbi ya tsunami yanaweza kurudi tena huku matangazo ya tahadhari yakiendelea kutolewa hata baada ya saa nzima tangu tahadhari ya kwanza itolewe.

Matetemeko mengine kadhaa madogomadogo yalilipiga eneo hilo.

Vinu vya  nyuklia viko salama

Msemaji wa serikali ya japan, Yoshimasa Hayashi, aliwaambia waandishi wa habari kwamba vinu vya nyuklia kwenye eneo hilo havijaripoti tukio lolote lisilo la kawaida, ingawa ni "muhimu kwa watu wa maeneo ya mwambao kuhama haraka iwezekenavyo."

Matangazo ya hadhari ya tsunami nchini Japan.
Matangazo ya hadhari ya tsunami nchini Japan.Picha: Eugene Hoshiko/AP/picture alliance

Mawimbi ya tsunami ya ukubwa wa mita tatu yalipiga kwenye mwambao wa Nigita na maeneo mengine ya jirani na hapo.

Soma zaidi: Umoja wa Ulaya waondoa vikwazo vya vyakula vya Japan

Serikali ya Japan imeanzisha kituo maalum cha dharura kukusanya taarifa za matetemeko na tsunami na kuzisambaza haraka kwa raia, kwa mujibu wa Waziri Mkuu Fumio Kishida, aliyerejelea onyo la kuhamwa haraka kwa maeneo yaliyoathirika.

Japan ni taifa lililo kwenye eneo lenye uwezekano mkubwa wa kukumbwa na tsunami. Mwezi Machi 2011, tetemeko kubwa na tsunami yalisababisha madhara makubwa kwenye kinu kimoja cha nyuklia.

Vyanzo: AFP, AP, Reuters