1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump kuongeza bajeti ya ulinzi

Yusra Buwayhid
28 Februari 2017

Ikulu ya Marekani inataka kuongeza bajeti ya ulinzi kwa kiasi cha dola bilioni 54. Kulingana na Rais Donald Trump, ongezeko hilo litapatikana baada ya kupunguzwa bajeti ya misaada ya nchi za nje inyotolewa na Marekani.

https://p.dw.com/p/2YMh2
USA Präsident Donald Trump bei der Conservative Political Action Conference  Oxon Hill Maryland
Picha: Getty Images/Pool/O. Douliery

Rais wa Marekani Donald Trump anapanga ongezeko kubwa la kihistoria katika bajeti ya ulinzi wa nchi, lakini Wademokrat na Warepublican ndani ya Baraza la Congress la Marekani, ambao atawahitaji kuiidhisha, wote wanaipinga bajeti hiyo inayopendekezwa na Trump.

Bajeti inayopendekezwa na Trump inatarajia kuongeza matumizi ya wizara ya ulinzi ya Marekani Pentagon kwa asilimia 10, na kuifanya bajeti jumla kuwa dola bilioni 603. Fedha hizo zitapatikana kwa kupunguza matumizi ya programu nyengine za serikal,i za ndani na nje ya nchi, ili zipatikane dola bilioni 54 ambazo ni sawa na asilimi hiyo 10.

"Tutafanya mengi kwa matumizi madogo. Serikali itatumia bajeti ndogo ili iwajibike zaidi kwa wananchi wake. Tunaweza kufanya mambo makubwa zaidi kwa fedha tunazozitumia. Tuna madeni ya dola trilioni 20, hebu lifikirieni hilo, serikali lazima ijifunze kukaza mkanda, kitu ambacho familia zote za Marekani zimelazimika kujifunza kufanya, kwa bahati mbaya," amesema Rais Donald Trump, akizungumza akizungumza na magavana wa Marekani katika Ikulu ya White House.

Trump ameongeza kuwa matumizi zaidi yatakuwa katika sekta ya miundombinu. Trump anasema hafanyi hivyo kwa kutaka tu, bali barabara pamoja na madaraja ya Marekani yote hayana usalama kwa sasa.

Mpango huo wa bajeti ambao bado upo katika hatua za awali unakuja kabla ya hotuba yake ya kwanza mbele ya Baraza la Congress ambayo itafanyika leo hii.

Kwa mujibu wa taarifa za shirika la habari la CNN, zaidi ya majenerali wastaafu 120, wamemshauri Trump kutopunguza bajeti  katika programu za kidiplomasia pamoja na misaada ya maendeleo kwa nchi za nje.

USA Trump will Verteidigungsetat erhöhen
Rais Donald Trump, akizungumza na magavana wa MarekaniPicha: REUTERS

Jenerali mstaafu David Petraeus, Mkurugenzi wa zamani wa Shirika la Ujasusi Marekani CIA, na Maafisa wawili wa baraza la mawaziri pamoja na Mkuu wa zamani wa jeshi la wanamaji Admeri James Stavridis, ni miongoni mwa wale waliomsisitiza Trump kutotekeleza vitisho vyake vya kupunguza bajeti katika sekta alizozidhamiria.

CNN imewanukuu wanajeshi hao wakisema katika barua yao kwa viongozi wa baraza la Congress, Maafisa wawili baraza la mawaziri, pamoja na mshauri wa usalama wa Trump kuwa bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje ni muhimu sana kwa usalama wa Marekani.

Mpango huo wa Trump pia umekosolewa vikali na upande wa Wademocrat, ambao wana uwezo wa kuupinga usipitishwe. Na kwa upande wa Warepulican wenzake mpango huo umepokelewa kwa hisia tofauti kuna wanaomuunga mkono Trump, na wenye wasiwasi na mpango wake huo.

Kuna uwezekano wa mpango wa bajeti wa Rais Trump ambao bado upo katika hatua za awali ,ukafanyiwa marekebisho makubwa hadi pale bajeti rasmi itakapotolewa mwezi Mei. Bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2018 itaanza kutumika rasmi Oktoba mosi.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/ape/afpe/dw

Mhariri: Bruce Amani