1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump ateuliwa rasmi kuwania urais kwa Republican

Mohammed Khelef20 Julai 2016

Sasa ni rasmi kuwa bilionea Donald Trump ndiye mgombea wa urais wa Marekani kwenye uchaguzi wa mwezi Novemba, baada ya mkutano mkuu wa chama cha Republican kulipitisha jina lake kwa ushindi mkubwa.

https://p.dw.com/p/1JSOS
Donald Trump akiwahutubia wajumbe wa mkutano mkuu wa Republican kwa njia ya vidio.
Donald Trump akiwahutubia wajumbe wa mkutano mkuu wa Republican kwa njia ya vidio.Picha: picture-alliance/dpa/D. Maxwell

Mara tu baada ya Trump kupitishwa rasmi, viongozi wa baraza la Congress kutoka Republican walijikuta wakitumia muda wote kusaka ujenzi mpya wa chama chao na pia kumshambulia mgombea wa chama cha Democrat, Hillary Clinton, kuliko muda waliotumia kumuelezea mgombea wao.

Spika wa baraza la wawakilishi, ambaye ndiye aliyelitambulisha rasmi jina la Trump kwenye mkutano huo Cleveland, Paul Ryan, amewataka wajumbe wote kuungana pamoja, baada ya mgawanyiko mkubwa ndani ya chama dhidi ya Trump.

"Sasa mnasemaje? Mnasemaje kuhusu kukiunganisha chama hiki katika wakati huu muhimu sana ambapo umoja ndio kila kitu. Tuelekeze mapambano yetu sasa dhidi ya wapinzani wetu tukiwa na mawazo bora zaidi. Tukashambulie na tubakie kwenye eneo la mashambulizi," alisema Ryan.

Kampeni za kutaka Republican isimchaguwe Trump zilishindwa kwenye hatua zake za awali. Maandamano ya kumpinga nje ya jengo la mkutano na majibizano kati ya waungaji mkono na wapinzani yalizimika mara tu baada ya kutangazwa rasmi, huku wajumbe waliomkataa wakitoka ukumbini.

Nina uhakika wa kushinda urais

Mwenyewe Trump amewaambia maelfu ya wajumbe wa chama chake kwamba ana hakika atashinda kwenye uchaguzi wa urais, huku akisema anaona fahari kuwa mteule wao. Akizungumza kwa njia ya vidio amewashukuru watoto wake kumuunga mkono tangu hatua za awali, na pia akamsifu mteule wake wa nafasi ya makamu wa rais, Gavana Mark Pence wa Indiana, huku akiendeleza kaulimbiu yake ya kuirejeshea Marekani hadhi yake ya zamani.

"Huu utakuwa uongozi ambao unawaweka watu wa Marekani kwenye nafasi ya kwanza. Tutazirejesha ajira zetu, tutalijenga upya jeshi letu lililoporomoshwa na kuwahudumia wanajeshi wetu wa zamani, tutakuwa na mipaka imara, tutawaangamiza kundi la Dola la Kiislamu, tutarejesha utawala wa sheria."

Wajumbe wa mkutano mkuu wa Republican katika uteuzi wa mgombea wao wa urais mjini Cleveland.
Wajumbe wa mkutano mkuu wa Republican katika uteuzi wa mgombea wao wa urais mjini Cleveland.Picha: picture-alliance/newscom/P. Marovich

Hadi kufikia hatua hii, bilionea huyo ambaye hana uzoefu wowote wa kisiasa, alishawaangusha waliokuwa wapinzani wake 16 kuwania tiketi ya Republican, wakiwemo magavana na maseneta waliokuwa na uzoefu mwingi kwenye tabaka la wanasiasa wa Republican.

Kutokuwa kwake mtu wa ndani ya chama, wanasema wachambuzi, ndiko ambako kunawafanya hata waungaji mkono wake kutumia muda mrefu zaidi kuzungumzia mapungufu ya mgombea mtarajiwa wa Democrat, Hillary Clinton, kuliko ule wanaoutumia kumjenga Trump.

Spika wa Baraza la Wawakilishi, Ryan, kwa mfano, alimtaja Trump mara mbili tu kwenye hotuba yake ya kumtambulisha rasmi kwa wajumbe wa mkutano mkuu.

Trump ataambatana na mgombea wake mwenza kuhutubia mkutano huo usiku wa Alhamis (21 Julai).


Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Caro Robi