1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump ataka Urusi irejeshwe kundi la G8

Iddi Ssessanga
9 Juni 2018

Rais wa Marekani Donald Trump ametoa wito mpya wa kuirudhisha Urusi katika kundi la mataifa yaliostawi zaidi kiviwanda duniani, licha ya kukumbana na upinzani mkali kwa pendekezo lake kutoka kwa wenzake nchini Canada.

https://p.dw.com/p/2zDQl
G7 Gipfel in Charlevoix Kanada Trump PK
Picha: picture-alliance/AP Photo/E. Vucci

"Nadhani ingekuwa jambo la manufaa kuirejsha Urusi," Trump aliwaambia waandishi habari kabla ya kuondoka kwenye mkutano wa kilele wa kundi la mataifa saba yalioendelea zaidi kiviwanda.

"Nadhani ingekuwa vizuri kwa Urusi, Nadhani lingekuwa jambo zuri kwa Marekani, nadhani ingekuwa vizuri kwa mataifa yote ya kundi la sasa la G7. Nadhani G8 ingekuwa bora. Nadhani kuirudisha Urusi lingekuwa jambo zuri. Tunatafuta amani duniani. Hatutafuti kucheza michezo."

Pendekezo la Trump la kuirejesha Urusi ndani ya kundi -- ambalo alilitolea mjini Washington muda mfupi kabla ya kuondoka kwenda Canada -- lilikataliwa mara moja na wanachama wa G7 kutoka barani Ulaya, zikiwemo Uingereza, Ufaransa na Ujerumani katika siku ya kwanza ya mkutano huo.

Urusi ilitimuliwa katika kundi lililokuwa wakati huo G8 baada ya hatua yake ya kulitwaa kimabavu eneo la Crimea mwaka 2014, hatua iliolaaniwa pakubwa kama shambulizi dhidi ya mamlaka ya kujitawala ya Ukraine.

G7-Gipfel in Kanada
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, akiwa na mazungumzo na viongozi wenzake; Donald Trump wa Marekani (katikati), Emmanuel Macron wa Ufaransa (kulia), na waziri mkuu wa Canada Justin Trudeau.Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Licha ya matamshi ya Trump waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov alisema Jumamosi kuwa Moscow inafurahia kushirikiana na kundi kubwa zaidi la G20, na kwamba haijawahi kumuomba yeyote kuirejesha kwenye kundi la mataifa saba.

Italia nayo yataka Urusi irejeshwe

Waziri mkuu wa Italia Guiseppe Conte pia alisema anatumai kundi hilo la mataifa saba litaipokea tena Urusi mapema iwezekanavyo, lakini akaongeza kuwa Italia haitaki kuondolewa kwa vikwazo dhidi ya Urusi ndani ya "usiku mmoja".

"Italia inadhani ni muhimu kuwa na mazungumzo na Urusi lakini hii haimaanishi kwamba mfumo w vikwazo unaweza kuondolewa ndani ya usiku mmoja. Mfumo wa vikwazo umeunganishwa na makubaliano ya Minsk ambayo hayatekelezwa kikamilifu," Conte aliwaambia waandishi habari kandoni mwa mkutano huo.

Mazungumzo ya tija

Wakati huo huo, rais Trump amesema mazungumzo yake na wenzake wa kundi la G7 kuhusu biashara yalikuwa ya tija na kwamba angependelea ulimwengu usio na ushuru ikiwa mataifa mengine yanaitendea Marekani kwa haki.

G7 Gipfel in Charlevoix Kanada Trump PK
Mshauri mkuu wa kiuchumi wa ikulu ya White House Larry Kudlow, na mshauri mkuu wa usalama wa taifa John Bolton wakitazama wakati rais trump alizungumza na waandishi habari mjini La Malbaie, Quebec, Canada.Picha: picture-alliance/AP Photo/E. Vucci

Akizungumza na waandishi habari kabla ya kuondoka Quebec na kuelekea Singapore kuhudhuria mkutano wa kilele wa nyuklia na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un, Trump alikanusha kuwa mkutano wa G7 ulikuwa wa kishari.

"Hakuna ushuri, hakuna vikwazo.Hivyo ndivyo inavyotakikana. Na hakuna ruzuku. Na nimesema pia 'hakuna ushuru," Trump alisisitiza, wakati akitetea uamuzi wake wa kuongeza viwango vya ushuru kwenye bidhaa za chuma na bati zinazounzwa nchini Marekani.

"Tulikuwa na mazungumzo yenye tija kubwa kuhusu haja ya kuwa na bishara huru na ya haki," alisema. "Tunataka na kutaraji mataifa mengine kufungua kwa haki zaidi masoko yao kwa bidhaa za Marekani, na kwamba tutachukuwa hatua zozote zinazostahiki kulinda sekta na wafanyakazi wetu dhidi ya matendo yasio ya haki, ambayo ni mengi. Lakini tunayashaghulikia taratibu lakini kwa uhakika."

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,rtre,

Mhariri: Zainab Aziz