1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump aruhusu kutolewa kwa nyaraka za siri za FBI

Sekione Kitojo
3 Februari 2018

Rais Donald Trump na washirika wake katika chama cha Republican wametoa nyaraka zenye utata za kumbukumbu wakilishutumu shirika la upepezi wa  jinai FBI kwa upendeleo na matumizi  mabaya ya madaraka.

https://p.dw.com/p/2s3w1
USA PK Präsident Donald Trump nach Schießerei in Alexandria, Virginia
Picha: Getty Images/C. Somodevilla

Hali hiyo inazidisha  mapambano   kati ya  Ikulu  ya  White House na  waendesha  mashitaka  wanaochunguza kundi  la kampeni  ya rais.

Trump  alikaidi mkurugenzi  wake  wa  FBI  na  wizara  ya  sheria  na  kuamuru kutolewa  hadharani  waraka wenye  kurasa  nne  wa  Republican , ambao unaonesha  matumizi  mabaya  ya  madaraka  na  kuelemea  chama  kimoja katika  shirika  hilo  kubwa  nchini  Marekani  linalolinda  haki.

Robert Mueller
Mkurugenzi wa FBI Robert MuellerPicha: picture-alliance/AP/C. Dharapak

"Nafikiri ni fedheha. Kile  kinachoendelea  katika  nchi  hii, nafikiri  ni fedheha," Trump  aliyeonekana  kuwa katika  hali  ya kutofurahishwa, alisema wakati  akitangaza  uamuzi  wake  wa  kuruhusu nyaraka  hizo za kumbukumbu  kutolewa  hadharani. "Watu  wengi wanapaswa  kuona  aibu na  zaidi  ya  hapo."

Wademocrats  na  baadhi  ya  Warepublican  wamelalamika  kuwapo  na mchezo  mchafu kuhusiana  na  waraka  huo, wakipuuzia  kutolewa  kwake kuwa  ni  kama sarakasi  tu, na  juhudi  nyingine  dhaifu  kuvuruga uchunguzi kuhusiana  na  mahusiano  kati  ya  timu  ya  kampeni  ya  Trump  na  Urusi.

Wanadai  waraka  huo , ulioandikwa  na  Devin Nunes, afisa  wa  mpito  wa Trump, mbunge  na  mwenyekiti  wa  kamati  ya  bunge  ya  ujasusi, ina matundu  makubwa. FBI  binafsi imesema  ina "wasi wasi  mkubwa" na usahihi  wa  waraka  huo.

Devin Nunes
Muandishi wa waraka huo muhimu Devin NunesPicha: picture alliance/AP Photo/P.M.Monsivais

Kutupiana  lawama

Waraka  huo unadai kwamba  utafiti  uliogharamiwa  na  chama  cha Democratic  ulisababisha  FBI kufanya upelelezi dhidi  ya  msaidizi  wa zamani  wa  Trump, Carter Page.

Katika  taarifa , afisa  wa  habari  wa  Ikulu  ya  Marekani  Sarah Sanders alisema  waraka  huo, "unatoa maelezo   yenye  wasi  wasi  mkubwa  juu  ya kuaminika  kwa maamuzi  yaliyofanywa   katika  ngazi  ya  juu  ya  wizara ya sheria  na  FBI.

USA Jared Kushner Berater und Schwiegersohn von Donald Trump
Mkwe wa Donald Trump Jared KushnerPicha: Getty Images/R. Sachs

Mtoto  wa  kiume  wa  Trump  Don Jr aliandika  katika  ukurasa  wa  Twitter kwamba inapaswa  kuwa  "mchezo  umekwisha" kwa  uchunguzi  wa  Urusi.

Uongozi  wa  Trump  wa  mwaka  mmoja  sasa  umegubikwa  na  madai kwamba  wasaidizi  wake  kadhaa, ikiwa  ni  pamoja  na  Don Jr  na  mkwe wake  wa  kiume  Jared Kushner , huenda  walishirikiana  na  serikali  ya Urusi  kumwangusha  mgombea  wa  chama  cha  Democratic Hillary Clinton.

Mshauri  maalum Robert Mueller tayari  amewataja  maafisa  wawili  ikiwa  ni pamoja  na  mwenyekiti  wa  kampeni  ya  Trump Paul Manafort , na  maafisa wengine  wawili  kwamba  wamekiri  kudanganya  kwa  wachunguzi, ikiwa  ni pamoja  na  mshauri  wa zamani  wa  usalama  wa  taifa Michael Flynn.

USA - Ermittlungen zur Russland-Affäre - Paul Manafort
Mwenyekiti wa kampeni ya Trump katika uchaguzi Paul ManafortPicha: picture alliance/AP Photo/C. Kaster

Rais  Trump  mwenye  umri  wa  miaka  71 amekana  madai  hayo  na kusema  ni  taarifa  za  uongo  na  mpango  wa  Wademocrat. Mueller anatarajiwa  hivi  karibuni  kumtaka  atoe ushahidi chini  ya  kiapo juu  ya  kile anachokifahamu.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe

Mhariri: Yusra Buwayhid