1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump airudisha Cuba kati ya nchi zinazofadhili ugaidi

12 Januari 2021

Utawala wa Trump umeirudisha Cuba katika orodha ya ‘nchi zinazofadhili ugaidi‘ na kuiwekea vikwazo vipya vinavyoweza kukwamisha ahadi ya Biden kufufua uhusiano na serikali ya kikomunisti katika nchi hiyo ya kisiwani. 

https://p.dw.com/p/3no4R
Rais wa Marekani, Donald Trump
Rais wa Marekani, Donald TrumpPicha: Yuri Gripas/dpa/picture-alliance

Waziri wa nchi za nje wa Marekani Mike Pompeo, ametangaza hatua hiyo jana Jumatatu akitaja ushirikiano kati ya Cuba na waasi wa Colombia, ushirikiano wa Cuba na serikali ya siasa za mrengo wa kati ya Venezuela pamoja na hatua ya Cuba kuwakaribisha wakimbizi wa Marekani kuwa miongoni mwa sababu zilizowafanya kuchukua hatua hiyo.

Suala la kuitangaza Cuba kuwa taifa linalofadhili ugaidi limejadiliwa kwa miaka mingi na ni miongoni mwa hatua kadhaa za mwisho za sera ya nchi za nje ambazo utawala wa Trumpunafanya kabla ya Biden kuchukua urais Januari 20.

Cuba na Marekani: Marafiki walio na nyuso mbili

Kuiondoa Cuba kwenye orodha ya nchi zinazofadhili ugaidi ilikuwa mojawapo ya mafanikio makubwa ya sera za kigeni za rais wa zamani wa Marekani Barrack Obama alipoimarisha uhusiano na kisiwa hicho, hatua ambayo pia iliungwa mkono na aliyekuwa makamu wake Joe Biden.

Mike Pompeo, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani
Mike Pompeo, waziri wa mambo ya nchi za nje wa MarekaniPicha: Getty Images/C. Somodevilla

Awali uhusiano kati ya nchi hizo ulivunjika Fidel Castro alipochukua mamlaka mnamo 1959.

Reynaldo Oliva, raia wa Cuba mwenye umri wa miaka 57 ni miongoni mwa wale ambao wameukosoa uamuzi wa utawala wa Trump.

"Mtizamo wangu kama raia wa Cuba ni ni kwamba, Rais Trump hana tena suluhisho, na anapaswa kukabidhi silaha zake. Hataki kuzikabidhi badala yake anataka kuendelea kuwa kero kwa taifa letu.” Amesema Oliva.

Trump abatilisha maamuzi yaliyofanya na Obama?

Kama alivyofanya mkataba wa Iran kuhusu nyuklia, Rais Trump aliamua kubatilisha maamuzi kadhaa ya Obama kuhusu Cuba. Amechukua msimamo mkali dhidi ya Cuba na kuirudishia vikwazo ambavyo utawala wa Obama ulilegeza au uliondoa pale pande hizo mbili zilirejesha uhusiano kamili wa kidiplomasia mwaka 2015.

Maoni: Mwanzo mpyakwa Cuba?

Tangu Trump achukue madaraka, baada ya kampeni yake iliyoshambulia uamuzi wa Obama kurejesha uhusiano na Cuba, uhusiano kati ya Marekani na Cuba umekuwa ukizidi kuwa wa mkwaruzano.

Kando na shutuma dhidi ya Cuba kuwa inamuunga mkono rais wa Venezuela Nicolas Maduro, utawala wa Trump pia umeilaumu Cuba kuhusika katika mashambulizi ya sauti ambayo yamewaacha makumi ya wanadiplomasia wa Marekani mjini Havana, Cuba kuwa na majeraha ya ubongo tangu mwisho wa mwaka 2016.

Rais wa zamani wa Marekani (kushiti) na rais wa Cuba Raul Castro wakati w a mkutano wao wa kwanza mjini Havana Cuba Machi 21.2016
Rais wa zamani wa Marekani (kushiti) na rais wa Cuba Raul Castro wakati w a mkutano wao wa kwanza mjini Havana Cuba Machi 21.2016Picha: Reuters/C.Barria

Marekani yailaumu Cuba kwa kisiki dhidi ya juhudi zake kisheria

Kwenye taarifa, Pompeo amesema hatua yao inaiwajibisha tena serikali ya Cuba na kwamba inatuma ujumbe dhahiri kwa utawala wa Castro kukoma kufadhili ugaidi wa kimataifa na kuwa kisiki dhidi ya juhudi za kisheria za Marekani.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Cuba Bruno Rodriguez ameshutumu hatua hiyo ya Marekani. Kwenye ukurasa wa Twitter ameandika kwamba hatua ya Marekani kufuata masilahi yake ya kisiasa hutambuliwa na wale ambao kwa kweli wana wasiwasi kuhusu ugaidi na waathiriwa wa ugaidi.

Mwenyekiti mpya wa kamati ya bunge kuhusu mambo ya nchi za nje nchini Marekani Gregory Meeks amesema hatua hiyo ya utawala wa Trump haitasaidia Wacuba, bali inalenga tu kufunga mikono ya utawala wa Biden.

Orodha ya Marekani ya nchi zinazofadhili ugaidi

Vikwazo vya hivi karibuni dhidi ya Cuba, vinaiweka pamoja na Korea Kaskazini, Syria na Iran kama nchi pekee kwa sasa ambazo zinachukiwa kufadhili ugaidi

Kufuatia tangazo hilo la Jumatatu, safari nyingi kutoka Cuba zitazuiwa. Kuirudisha Cuba katika orodha hiyo kutazuia pakubwa wawekezaji kutoka nje ambao watakuwa katika hatari ya kushtakiwa na Marekani, hadi pale utawala wa Biden utakapoitathmini upya. Hiyo inamaanisha hatua hiyo inaweza kudumu kwa miezi kadhaa.

Mara kwa mara, Cuba imekataa kuwarudisha nyumbani Wamarekani waliokimbia nchi yao, na ambao Cuba imewapa hifadhi.

 Mnamo mwezi Mei 2020, wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani iliiongeza Cuba katika orodha ya nchi ambazo hazishirikiani na mipango ya Marekani katika kupambana na ugaidi.

(APE, AFPE)