1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump adaiwa kufichua siri za kijasusi kwa Urusi

Caro Robi
16 Mei 2017

Rais wa Marekani Donlad Trump alifichua taarifa nyeti za kijasusi kwa waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov kuhusu operesheni iliyokuwa inapangwa dhidi ya wanamgambo wa kundi la Dola la Kiislamu IS.

https://p.dw.com/p/2d1oG
USA Treffen zwischen Trump und Lavrov
Picha: picture alliance/dpa/A. Shcherbak

Katika sakata jingine linaloukumba utawala wa Rais Trump ambaye hajakaa madarakani kwa muda mrefu, Gazeti la Washington Post limeripoti kuwa Rais Trump alifichua taarifa za siri kwa Urusi. Ikulu ya White House imezitaja taarifa hizo kuwa za uongo. Tangu kuingia madarakani mwezi Januari, Trump amejikuta akijitosa kutoka sakata moja hadi jingine.

Katika taarifa zilizochapishwa hapo jana, Washington Post imenukuu duru kutoka kwa maafisa wa zamani na wa sasa wa Marekani ambao wamesema Rais Trump alitoa taarifa nyeti za kijasusi kwa Lavrov na balozi wa Urusi nchini Marekani Sergey Kislyak wakati walipokutana kwa mkutano wiki iliyopita katika ikulu ya mjini Washington.

Kuvujishwa kwa taarifa kutahujumu uhusiano

Taarifa hizo zilitoka kutoka kwa mmoja wa washirika muhimu wa Marekani anayehusika katika vita dhidi ya kundi hilo la kigaidi ambaye hakuipa Marekani ruhusa ya kuzitoa taarifa hizo zinazohusiana na mipango ya kigaidi ya kundi la wanamgambo wenye itikadi kali wa Dola la Kiislamu IS kwa Urusi.

USA McMaster: Bericht über Trumps Geheimnis-Weitergabe ist falsch
Mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani H.R: McMasterPicha: Getty Images/M. Wilson

Licha ya kuwa Rais ana mamlaka ya kufichua hata taarifa nyeti za kijasusi, katika kisa hiki hakushauriana na mshirika aliyezitoa taarifa hizo. Kulingana na maafisa wa kijasusi ambao hawakutaka kutambulika, kutolewa kwa taarifa hizo kunahujumu ushirikiano wa kubadilishana taarifa za kijasusi kati ya Marekani na washirika.

Mshauri wa masuala ya kitaifa ya usalama wa utawala wa Trump H.R McMaster amewaambia waandishi wa habari kuwa taarifa hizo za kuvujishwa kwa taarifa nyeti za kijasusi si za kweli akiongeza kuwa Trump na viongozi hao wa Urusi walitathmini vitisho mbali mbali vya kiusalama ikiwemo kitisho kinacholenga safari za anga.

Ikulu ya Rais baadaye ilitoa taarifa kutoka kwa waziri wa mambo ya nje Rex Tillerson ambaye alifafanua kuwa mkutano huo wa wiki iliyopita ulituwama katika suala la kupambana na ugaidi.

Trump ajikuta kwa kashfa moja baada ya nyingine

Licha ya maafisa wa ngazi ya juu wa utawala wa Trump kukanusha taarifa hizo zilizoripotiwa na Washington Post, wabunge wa chama cha Democratic wakiongozwa na Dick Durbin wameitaja mienendo ya Trump kuwa hatari na isiyojali.

Weißes Haus Trump trifft Lawrow
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavron na Rais Donald TrumpPicha: picture-alliance/dpa/AP/Russian Ministry of Foreign Affairs

Mbunge wa chama cha Republican Bob Corker anayesimamia kamati ya Seneti ya masuala ya kigeni ameyataja madai hayo ya kutia wasiwasi mkubwa iwapo yatabainika kuwa ya kweli.

Hayo yanajiri siku chache baada ya Trump kushutumiwa vikali baada ya kumfuta kazi mkurugenzi wa shirika la upelelezi James Comey katika mazingira ya kutatanisha wakati ambapo alikuwa akifanya uchunguzi kuhusu madai ya Urusi mwaka uliopita kuingilia uchaguzi wa rais wa Marekani.

Duru zinaarifu kuwa baada ya Trump kubobokwa taarifa hizo za siri kubwa, maafisa waliyaarifu mara moja shirika la kijasusi la Marekani CIA na shirika la usalama wa taifa ambayo yana makubaliano na mashirika ya kijasusi ya nchi washirika kote duniani na kuwajulisha kilichojiri.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/Afp

Mhariri:Josephat Charo