1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Tishio la Marekani kusimamisha msaada wa kijeshi kwa Ukraine

Saleh Mwanamilongo
4 Oktoba 2023

Wanajeshi wa Ukraine hivi karibuni watakosa risasi na vifaa muhimu vya kivita ikiwa wafuasi wenye msimamo mkali wa chama cha Republican nchini Marekani watafanikiwa kusimamisha msaada wa kijeshi wa Marekani kwa Ukraine.

https://p.dw.com/p/4X6ne
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken akitembelea eneo la hifadhi ya sialaha mjini Kyiv
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken akitembelea eneo la hifadhi ya sialaha mjini KyivPicha: Brendan Smialowski/AP/picture alliance

Wataalamu wamesema hali hiyo itadhoofisha operesheni za ardhini na kupunguza uwezo wa Ukraine wa kujilinda dhidi ya mashambulizi ya Urusi.

Maafisa wakuu wa Marekani wamesisitiza mara kwa mara kuwa Marekani itaiunga mkono Kyiv kwa nguvu na mali na Washington imetoa msaada wa kiusalama wa dola bilioni 43 tangu Urusi ilipoivamia Ukraine Februari 2022. Msaada huo ni zaidi ya nusu ya jumla ya wafadhili wote wa Magharibi.

Soma pia: Marekani yataka Ukraine isaidiwe na silaha zaidi

Lakini upinzani wa chama cha Republican unaongoza bunge la Congress umetaka kuondoa ufadhili mpya kwa Ukraine.

Wabunge wa Republican wanashikilia kwamba uungwaji mkono unaoendelea wa Marekani kwa Ukraine hauna uhakika. Mark Cancian, mshauri mkuu katika Kituo cha Mafunzo ya Kimkakati na Kimataifa amesema ni jambo la kusikitisha kwa Waukraine ikiwa misaada ya Marekani itasitishwa.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy akikutana na wanajeshi katika uwanja wa vita
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy akikutana na wanajeshi katika uwanja wa vitaPicha: Ukrainian Presidential Press Office/UPI Photo/Newscom/picture alliance

Aliendelea kusema kuwa jeshi la Ukraine litadhoofika na hatimaye labda kusambaratika ingawa linaweza kushikilia tu kwa kujihami.

Marekani imetoa silaha nzito kusaidia Kyiv kupambana ili kurejesha eneo lililotekwa na Urusi. Marekani imetoa kuanzia risasi ndogo ndogo za silaha na mizinga hadi magari, virusha roketi vya hali ya juu, vifaru na vifaa vya kusafisha mabomu ya kutegwa ardhini.

Wanajeshi walio katika vita wanahitaji mtiririko unaoendelea wa silaha na vifaa na zana ili kuchukua nafasi ya kile kilichoharibiwa au tayari kutumika, alisema Cancian.

Iwapo misaada ya Marekani itasitishwa kabisa jambo ambalo Ikulu ya Marekani inasisitiza kuwa halitafanyika athari hazitokuwa za mara moja, ikizingatiwa kwamba msaada ulioidhinishwa hapo awali bado uko mbioni.

Ni zipi athari iwapo Marekani itasitisha msaada wa silaha kwa Ukraine? 

Mark Cancian alisema inaweza kuchukua pengine wiki kadhaa kabla ya kuona athari kwenye uwanja wa vita, na Moscow inaweza kukosa kufaidika na hatua hiyo kwa sababu hata wanajeshi wa Urusi pia wamechoshwa na vita.

Mbali na uwanja wa vita, kukomeshwa kwa misaada ya Marekani kutaacha pengo katika ulinzi wa anga wa Ukraine, ambao unaundwa na mifumo kutoka nchi nyingi. Ulinzi huu wa anga una jukumu muhimu katika kulinda raia na miundombinu ya Ukraine dhidi ya mashambulizi ya mara kwa mara ya droni na makombora ya Urusi.

Waziri wa ulinzi wa Marekani Lloyd Austin akisalimiana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy
Waziri wa ulinzi wa Marekani Lloyd Austin akisalimiana na Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyyPicha: Ukraine Presidency/Zumapress/picture alliance

James Black, mkurugenzi msaidizi wa wa kundi la utafiti wa ulinzi na usalama barani Ulaya RANDEurope amesema hauwezi tu kubadilisha mfumo mmoja wa ulinzi na silaha na mfumo mwingine ikiwa unafanya kazi kwa njia tofauti na kukabiliana na vitisho tofauti.

Hiyo inamaanisha nchi nyingi hasa za Ulaya zimetoa msaada wa kijeshi kwa Ukraine, na ingawa zinaweza kuongeza uungwaji mkono, lakini kuziba pengo litakaloachwa na Marekani itakuwa changamoto kubwa na ya muda mrefu kwa Ukraine.

Soma pia: Washirika wa Ukraine wakutana Ujerumani kujadili msaada zaidi 

Spika wa Bunge la Marekani Kevin McCarthy alisema wanachama wa chama chake cha Republican waliunga mkono shinikizo la kutaka kusitishwa usaidizi wa Marekani kwa Ukraine. Lakini kiongozi huyo alisema Ukraine itapata usaidizi pale tu kutakuweko na juhudi zaidi za usalama dhidi ya uhamiaji haramu kwenye mpaka wa Marekani na Mexico.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin ambaye alichukua jukumu muhimu katika kuunda muungano wa kimataifa kuunga mkono Ukraine, na kisha katika kuratibu usaidizi, alitoa wito mwishoni mwa juma kwa Congress kuchukua hatua.

Austin alisema wabunge wanapaswa kufanya vyema juu ya dhamira ya Marekani ya kutoa msaada unaohitajika haraka kwa watu wa Ukraine wanapopigana kulinda nchi yao dhidi ya nguvu za udhalimu.