1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Tisa wauwawa Afghanistan

Polisi nchini Afghanistan wamesema bomu lililotegwa ndani ya gari na kuegeshwa katika mlango wa chumba cha uwanja wa ndege mashariki mwa nchi hiyo limeripuka na kuuwa watu tisa.

Bomu liliotegwa garini laripuka na kuuwa watu 9

Bomu liliotegwa garini laripuka na kuuwa watu 9

Duru za hivi karibuni zinasema watu tisa wamekufa kutokana na mripuko huo ambao umetokea baada ya ghasia zilizofuatia kuchomwa kwa Koran, kitabu kitakatifu cha waumini wa kiislamu katika kambi ya jeshi ya Marekani. Hata hivyo hakukuwepo dalili zinazoonesha shambulizi hili lililotokea katika uwanja wa ndege wa Jalalabad lilikuwa na mafungamano na maandamano na ghasia hizo za kuchomwa kwa Koran.

Kundi la waasi wa Taliban limejigamba kuhusika katika shambulizi hilo ambalo wamesema ni hatua ya kulipiza kisasi kuchomwa kwa kitabu hicho. Obaidullah Talwar, afisa mkuu wa polisi Mashariki mwa Afghanistan amesema raia wengine 15 walijeruhiwa katika mlipuko huo.

Waasi wa Taliban

Waasi wa Taliban

Licha ya msamaha kutolewa na viongozi wa Marekani akiwemo Rais Barrack Obama, wanajeshi saba walijeruhiwa baada ya bomu kurushwa ndani ya kambi yao kaskazini mwa Afghanistan. Huku kukiwa hakuna dalili ya kukomesha ghasia nchini humo Balozi wa Marekani nchini Afghanistan amesema Marekani haitaondoa vikosi vyake nchini humo kabla ya muda uliopangwa.

Balozi huyo Ryan Crocker akizungumza na shirika la habari la CNN amesema kwa sasa kuna hali ya taharuki, Crocker amesema anadhani ni vyema kuacha ghasia zipoe na hali kurudi kama kawaida kabla ya kuendelea na kazi. Ryan Crocker amesema huu si wakati wa kuvunjika moyo na kuondoka nchini humo lakini ni wakati wa kuongeza juhudi zao na kuhakikisha kuwa kundi la kigaidi la Al Qaeeda halitarudi tena.

Katika makubaliano ya kimataifa vikosi vya jeshi la Marekani vinapaswa kumaliza muda wake Afghanistan ifikapo mwaka wa 2014.

Washauri waondolewa Afghanistan

Huku hayo yakiarifiwa Ufaransa na Ujerumani wamesema watawaondoa washauri wao kutoka taasisi za Afghanistan kufuatia kuuwawa kwa kupigwa risasi wanajeshi wawili wa NATO mjini Kabul. Nchi hizo mbili zimesema kuondoa washauri wake katika wizara tofauti nchini humo ni kwa ajili ya usalama.

Rais wa Afghanistan Hamid Karzai

Rais wa Afghanistan Hamid Karzai

Rais Hamid Karzai ametoa ripoti inayowasihi waandamanaji na vikosi vya usalama vya Afghanistan kusimamisha ghasia nchini humo huku akisema kuwa serikali yake inaendelea kuishinikiza Marekani kuwachukulia hatua kali waliotekeleza kitendo hicho.

Tangu kuanza kwa maandamano hayo wiki moja iliopita, watu zaidi ya 30 wameuwawa na wengine zaidi ya 200 kuujeruhwa vibaya. Miongoni mwa waliouwawa ni wanajeshi wawili wa Marekani ambao walipigwa risasi na askari wa Afghanistan aliyekuwa amejiunga na makundi ya waandamanaji.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Hillary Clinton amesema ghasia hizo ni lazima zisimamishwe.

Mwandishi Amina Abubakar

Mhariri:Gakuba, Daniel

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com