1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Theo Zwanziger-rais wa DFB atunzwa zawadi

2 Novemba 2009

Kwa vita dhidi ya ubaguzi viwanjani.

https://p.dw.com/p/KLnS
Theo Zwanziger (rais DFB)Picha: picture-alliance/ dpa

Werder Bremen ilitoka sare 2-2 na Nuremberg,imeparamia kileleni mwa Bundesliga wakati mabingwa mara kadhaa Bayern Munich hawakumudu zaidi ya sare kati yao na Stuttgart.

Rais wa DFB,Theo Zwanziger,atunukiwa zawadi ya Leo-Baeck ya Baraza la wayahudi,Ujerumani.

Liverpool imeteleza tena katika Premier League-Ligi ya Uingereza huku Chelsea ikiendelea kuongoza ikifuatwa na Manchester united nafasi ya pili.

Deratu Tulu wa Ethiopia, ashinda mbio za New York marathon upande wa wanawake wakati muamerika wa asili ya Eritrea anyakua taji la wanaume.

Katika Ligi ya Tanzania, simba imenguruma mbele ya Younga

, mjini Dar-es-salaam.

Tukianza na Ligi mashuhuri barani ulaya, Bayer Leverkusen, inaongoza sasa Bundesliga kwa pointi 1 kileleni licha ya kupoteza pointi 2 mwishoni mwa juma ilipotoka suluhu na Schalke 2:2.Mkwaju maridadi ajabu aliouchapa Toni Kroos na bao la kichwa la Stefan Kiessling,yaliiona Leverkusen ikiongoza kwa mabao 2:0.Lakini Kevin Kuranyi,alizima vishindo hivyo vya darini vya Leverkusen na kuwateremsha sakafuni kwa bao lake la dakika ya 88 ya mchezo lililosawazisha matokeo 2:2.

Werder Bremeniklihitaji bao la dakika ya mwisho kutoka kwa Aaron hunt kutoka pia sare mabao 2-2 dhidi ya Nuremberg na sasa imejongea nafasi ya pili kileleni .Borussia Mönchengladbach iliopo mkiani mwa Ligi ,ilitamba nyumbani mwa viongozi wa Ligi, Hamburg na kuondoka na ushindi wa mabao 3-2.Pigo hilo limeiteremsha chini Hamburg hadi nafasi ya tatu ikiwa na pointu sawa kama Bremen.

Mabingwa mara kadhaa wa Ujerumani,Bayern Munich ,wanaodai kwamba kabla ya mwisho wa mwaka huu watakuwa kileleni mwa Bundesliga, hawakumudu zaidi ya sare ya 0:0 na majirani zao Stuttgart.Munich ingawa ilidhibiti mchezo ,haikuona wavu wa lango la Stuttgart.

Kocha wa Bayern Munich, mdachi Van gaal, ambae amekuwa akiyumbayumba ,alisema :

"Naweza kuridhika na sare ya 0:0.Nadhani hatukutayarisha nafasi nyingi za kuweza kutia magoli na hivyo, hatujastahiki zaidi."

Matokeo hayo lakini ,hayataimarisha kiti chake kinacho regarega.Munich sasa, iko pointi 1 nyuma ya Hoffenheim ambayo ni timu pekee kati ya 3 ziliopo kileleni,kushinda mwishoni mwa wiki.Hoffenheim, ilitamba mbele ya Freiburg.

Bochum, licha ya kucheza chini ya kocha mpya, haikuepuka pigo jengine mara hii kutoka Frankfurt.Frankfurt, imejizatiti kati ya ngazi ya ligi wakati Bochum, inaendelea kuburura mkia kama Hertha Berlin. FC Cologne, imewavunja moyo mashabiki wake nyumbani waliotazamia pointi 3 Jumamosi kutoka kikapu cha mahasimu wao Hannover 96.Lakini, kwa mara nyengine tena, Hannover ilitamba Cologne na kuondoka na pointi zote 3 .Pigo hilo limeirejesha FC Cologne karibuni na mkia mwa ligi.

TUZO LA LEO-BAECK-PREIS KWA RAIS WA DFB- THEO SWANZIGER :

Rais wa Shirikisho la dimba la Ujerumani (DFB) Theo Zwanziger, ametunzwa zawadi ya 2009 ya "Leo-Baeck-Preis "na Baraza Kuu la wayahudi nchini Ujerumani.Akiwa rais wa DFB-shirikisho la mpira la Ujerumani, Bw.Zwanziger, amechangia mno kupiga vita chuki za kikabila ,ubaguzi na siasa kali za mrengo wa kulia katika mchezo wa mpira.Hiyo ndio sababu ya kupewa zawadi hiyo.

Bw.Theo Zwanziger ,atapokea zawadi hiyo keshokutwa Novemba 4 mjini Berlin.Kwa rais wa DFB, hii si zawadi ya kwanza kupewa,lakini tuzo la Leo-Baeck ndilo analo lithamini mno.

Bw.Swanziger, alisema kwamba,amesangazwa binafsi kupewa zawadi hiyo ambayo inashikamana na jina la mtu maarufu.Jinsi alivyosangazwa, Bw.Swazinger anajiuliza: "Nimefanya nini kubwa kustahiki zawadi hiyo ? "

Zawadi hii ya Leo-Baeck imeanza kutolewa tangu 1957 na miongoni mwa waliotunukiwa ni marais wa zamani wa Ujerumani ,Richard von Weizsäcker na Roman Herzog na halkadhalika, Kanzela Angela Merkel.

Zawadi ya "Leo-baeck" hupewa wale ambao wametenda mengi kwa Jumuiya ya wahayhudi humu nchini.Theo Zwanziger, ambae tangu 2004 ni rais wa Shirikisho la mpira la Ujerumani amechangia sana vita vya kupambana na chuki za kikabila katika viwanja vya mpira. Kwani, ubaguzi wa kikabila ni sumu kali ambayo mara kwa mara hutiwa wanadamu na daima ,kuna watu wanaopalilia sumu hiyo ya ukabila.Bw.Zwanziger ,mwanasheria mwenye umri wa miaka 64 na shirikisho lake la mpira la DFB, daima amekuwa usoni katika kujitwika dhamana hiyo katika jamii.

PREMIER LEAGUE:

Ama katika Premier League-Ligi ya Uingereza,FC Liverpool imeteleza tena ,kwani wamepatwa na pigo la 5 katika Premier League na wachezaji wake 2 kutimuliwa nje ya uwanja .Kama msumari wa moto juu ya donda, Liverpool ikasindikizwa nje ya uwanja na wachezaji wake 9 waliosalia kwa mabao 3-1 kikapuni.

Sasa Liverpool, iko nyuma kwa pointi 9 kutoka viongozi Chelsea waliposhinda kwa mbao 4-0 katika mechi yao na Bolton Wanderes. Manchester United bado wananyatia kutoka nafasi ya pili baada ya ushindi wao wa mabao 2-0 dhidi ya Blackburn Robers.Arsenal iko nafasi ya 3 ikiwa na jumla ya pointi 22 kufuatia ushindi wao dhidi ya Tottenham Hotsopur wa mabao 3-0.

Katika Serie A-Ligi ya Itali, mabao ya kipindi cha pili aliotia Milito na Maicon yaliisaidia Inter Milan kushinda kwa mabao 2:0 dhidi ya Livorno; na sasa wamefungua mwanya wa pointi 7 kileleni mwa Serie A.Na hiyo ni baada ya kuchezwa mapambano 11 tu ya Ligi.

Inter ilitiwa moyo kwa mahasimu wao Sampsdoria kumudu sare ya 0:0 na Bari. Juventus ilio nafasi ya pili ya ngazi ya ligi kama Sampdoria, walikuwa wakiongoza kwa mabao 2 nyumbani kabla Datolo kuipatia ushindi wa mabao 3-2.

Katika la Liga-Ligi ya Spain, mabingwa Fc Barcelona, wameteleza kidogo.Stadi wao Gerard Pique alilifumania lango lake mwenyewe sekunde ya mwisho ya mchezo na kufuta bao la stadi wao Seydou keita katika lango la Osasuna. Real madrid ilimpoteza stadi wake Raul katika kipindi cha kwanza walipopambana na Getafe ,lakini mabao 2 ya haraka ya muargentina Gonzalo Higuain yaliwapa Real ushindi wa mabao 2:0.

Ama huko Afrika Mashariki, katika changamoto kati ya mahasimu 2 wa mtaani-Simba na Younga mwioshoni mwa wiki, simba walinguruma kwa bao 1:0 na wako njiani kuhetimisha duru ya kwanza ya Ligi ya Tanzania wakiwa kileleni:

NEW YORK MARATHON:

Mbio za kila mwaka za New York marathon, mara hii upande wa wanaume, zilimalizikia ushindi wa Muamerika wa asili ya Eritrea, Meb Keflezighi.Muamerika huyo mwenye umri wa miaka 34, amekuwa wa kwanza tangu kupita miaka kiasi ya 20 kushinda NY marathon upande wa wanaume.Alichukua uraia wa Marekani ,1998.Keflezighi alimuacha bingwa mara 4 wa Boston marathon ,mkenya Robert Cheruiyot katika kituo cha maili 23 .Mkenya huyo mwishoe, alimaliza wapili.

Upande wa wanawake, taji lilikwenda Ethiopia,jirani ya Eritrea.Deratu Tulu, bingwa wa zamani wa olimpik katika mita 10.000 mjini Barcelona, alimkimbia mrusi Ludmila Petrova na kushinda New York marathon kwa muda wake wa masaa 2:28.52.

Mwandishi: Ramadhan Ali /DPAE/AFPE

Mhariri:Abdul-Rahman