Maandamano yamalizika.
14 Aprili 2009
Polisi ya Thailand imewafungulia mashkata viongozi watatu wa maandamano yaliyofanyika kuipinga serikali, yaliyomalizika leo baada ya wanajeshi kutishia kutumia nguvu.
Wakati huo huo mahakama imetoa hati ya kisheria ya kuwezesha kukamatwa kwa aliekuwa waziri mkuu wa Thailand Thaksin Shinawatra anaeishi nje ya nchi hiyo.
Waranti juu ya kukamatwa kwa bwana Shinawatra umetolewa pia kwa watu wengine 12 wanaomuunga mkono waziri mkuu huyo wa zamani.
Kufunguliwa mashtaka kwa viongozi hao watatu - wapinzani wa serikali ya Thailand, pamoja na waranti uliotelewa dhidi ya bwana Shinawatra kunafuatia kumalizika leo, kwa maandamano na harakati za kuipinga serikali ambapo wapinzani waliweza kuyadhibiti makao makuu ya serikali kwa muda wa takriban wiki tatu.
Kwa mujibu wa waranti uliotolewa , Shinawatra na watu wanaomuunga mkono wamechochea ghasia, na wamehatarisha amani; adhabu ya makosa hayo ni kifungo cha miaka mitano jela.
Katika maandamano ya kuipinga serikali yaliyochukua takriban wiki tatu, nchini Thailand watu wawili waliuawa na wengine 123 wamejeruhiwa.
Wapinzani wa serikali wanaomuunga mkono waziri mkuu wa zamani Shinawatra walipambana na wanajeshi .
Lakini mvutano huo umemalizika kwa amani na mji mkuu Bangkok umerejea katika utulivu kidogo.
Mwandishi:Mtullya.
Mhariri:Abdul-Rahman.
AFP.