1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TEHRAN: Iran yawaonesha wanamaji wa uingereza katika television,mmoja akiri walikosa

29 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCEZ

Televisheni ya Iran imeonesha mahojiano na askari pekee wa kike wa majini kati ya 15 wa Uingereza wanaoshikiliwa na nchi hiyo baada ya kuwakamata katika eneo la maji la nchi hiyo.

Mwanamaji huyo wa kike Faye Turney alikiri katika mahojiano hayo ya kwamba walikamatwa baada ya kuingia katika eneo la Iran bila ya ruhusa.Pia televisheni hiyo ya Iran ilionesha picha za askari wengine.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Margereth Beckett alielezea wasi wasi wake juu ya picha hizo.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Manouchehr Mottaki, amesema kuwa mwanamaji huyo wa kike huenda akaachiwa leo.

Wakati huo huo wanadiplomasia wanasema kuwa Uingereza imelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kutoa taarifa ya kutaka Iran iwaachie wanamaji hao mara moja.

Taarifa zinasema kuwa Uingereza imesambaza ombi hilo kwa wanachama 14 wa baraza hilo.

Uingereza imekuwa ikishikilia kuwa wanamaji hao walikuwa katika eneo huru la maji.

Naibu Mkuu wa jeshi la majini la Uingereza Admiral Charles Style amesema kuwa wanamaji hao walikuwa kiasi cha maili mbili kutoka eneo la Iran.