1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TEHRAN: Iran yataka mazungumzo ya kidiplomasia yatumike

3 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CCCv

Afisa mkuu wa maswala ya usalama nchini Iran amesema kwamba nchi yake inataka kuutatua mzozo kuhusu wanamaji 15 wa Uingereza waliokamatwa na kuzuiliwa nchini Iran kwa njia za kidiplomasia.

Ali Larijani ambae pia ni mpatanishi mkuu wa maswala ya nyuklia wa Iran amenukuuliwa na vyombo vya habari kwamba nchi yake haina haja ya kuwafikisha mahakamani wanamaji hao wa Uingereza.

Tehran imeshikilia msimamo wake kuwa wanamaji hao walivuka mipaka na kuingia katika pwani ya Iran huku Uingereza nayo ikisisitiza kuwa askari wake walikuwa katika eneo la pwani ya Irak wakitimiza majukumu yao kwa ruhusa ya Baghdad na umoja wa mataifa.

Awali radio ya Tehran ilitangaza kwamba wanamaji wote 15 wamekiri kuwa walikiuka sheria na kuingia katika pwani ya Iran bila ya idhini.

Wakati huo huo wizara ya mambo ya nje ya Marekani inatafuta taarifa zaidi kutoka kwa utawala wa Iran juu ya raia wake mmoja alieripotiwa kupotea kwa wiki kadhaa huko kusini mwa Iran.

Mtu huyo inaaminika kuwa ni afisa wa shirika la upelelezi la Marekani FBI ambae kwa mujibu wa serikali alikuwa nchini Iran katika ziara ya kibinafsi.