1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TEHRAN: Iran kuwaruhusu mamafisa wa kibalozi wa Uingereza kuwaona wanamaji wao itakapomaliza kuwahoji

28 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCEt

Iran imesema kuwa itawaruhusu wanadiplomasia wa Uingereza kuwatembelea wanamaji wa nchi hiyo inaowashikilia baada ya kumaliza kuwahoji.

Pia imeendelea kusisitiza kuwa wanamaji hao 15 inaowashikilia wako katika hali nzuri na wanapatiwa huduma zote za kibinaadam.Hata hivyo, imekataa kuelezea wapi inakowashikilia.

Iran inasema kuwa wanamaji hao waliingia katika eneo lake bila ya ruhusa na inachunguza kuona kama walikuwa katika safari za kipelelezi, lakini Uingereza, imesema kuwa askari hao walikuwa katika doria za kawaida.

Hayo yakiendelea, Ujerumani imejiunga na jumuiya ya kimataifa kutaka kuachiwa haraka kwa wanamaji hao.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani mjini Berlin imemuita Balozi wa Iran nchini Ujerumani na kutaka kuachiwa haraka kwa askari hao wa Uingereza.

Mjini London, Waziri Mkuu wa Uingereza Tony Blair ameionya Iran kuwa mzozo huo unaweza kuingia katika hatua tofauti, iwapo haitowaachia askari hao mara moja, kauli ambayo Iran imesema kuwa ni ya uchokozi.

Msemaji wa Tony Blair hata hivyo amesema kuwa Uingereza ingependelea kuona mzozo huo unamalizwa kwa njia ya kidiplomasia na kwamba haipendelei hatua za kijeshi wala kumtimua balozi wa Iran nchini Uingereza.