1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TEHRAN : Ahmedinejad adai Baraza la Usalama halina uhalali

15 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCIt

Rais Mahmoud Ahmedinejad wa Iran amesema leo hii kwamba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halina uhalali wakati chombo hicho cha dunia kikaribia kufikia makubaliano juu ya mpango wa vikwazo vipya dhidi ya nchi hiyo kutokana na mpango wake wa nuklea.

Ahmedinejad amesema katika hotuba wakati wa ziara yake ya siku mbili ya jimbo la kati la Yazd nchini Iran kwamba leo maadui wa wananchi wa Iran wanataka kulitumia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuzuwiya maendeleo na kupiga hatua kwa Iran.

Amesema lakini Baraza hilo la Usalama halina uhalali miongoni mwa watu duniani.

Maafisa kutoka nchi wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani inasemekana kuwa wamefikia muafaka juu ya kuzidisha vikwazo dhidi ya Iran.

Wajumbe kutoka nchi hizo wanasema azimio hilo la vikwazo viypya yumkini likawasilishwa kwa Baraza la Usalama leo hii na kupigiwa kura wiki ijayo.

Hizo ni jitihada za karibuni kabisa kuishawishi Iran kusitisha mpango wake wa nuklea ambao unazidi kutanuka kwa kukiuka azimio la Umoja wa Mataifa lililopitishwa hapo mwezi wa Desemba.

Mataifa ya magharibi yanahofu kwamba Iran inataka kutengeneza silaha za nuklea lakini Iran yenyewe inakanusha kwa kusema kwamba mpango wake huo ni kwa ajili ya dhamira za amani.