1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tamasha la Vitabu la Ujerumani lazingatia matumizi ya Dijitali

Admin.WagnerD5 Oktoba 2010

Hapo jana, Jumanne ya Oktoba 5, Ujerumani ilifungua tamasha lake kubwa la vitabu mjini Frankfurt. Mwito wa mara hii ni kuipa nafasi teknolojia ya mawasiliano kwenye utamaduni wa usomaji vitabu.

https://p.dw.com/p/PW3e
Mwanamke akipachika vitabu kwenye rafu ya vitabu katika mabanda ya Tamasha la Vitabu mjini Frankfurt lililofunguliwa jana, Jumanne 5 Oktoba 2010
Mwanamke akipachika vitabu kwenye rafu ya vitabu katika mabanda ya Tamasha la Vitabu mjini Frankfurt lililofunguliwa jana, Jumanne 5 Oktoba 2010Picha: AP

Rais wa Argentina, Cristina Kirchner, na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, jana walilifungua rasmi tamasha tamasha hili kubwa kabisa la vitabu duniani mjini Frankfurt. Mara hii, waandaaji wa tamasha wameweka mkazo kwenye matumizi ya teknolojia ya dijitali na mtandao ambayo sasa imekuwa sehemu ya ulimwengu wa vitabu.

Wachapishaji na waandishi vitabu zaidi ya 7, 500 kutoka nchi 111 duniani wanatarajiwa kuhudhuria tamasha hili na hivyo kuipa nafasi ya pekee teknolojia ya dijitali kutambuliwa kwenye fani hii kongwe katika historia ya mwanaadamu.

Mkurugenzi wa Tamasha hilo, Jürgen Boos aliwaambia waandishi wa habari kwamba, kusudi la kuweka mkazo kwenye mambo ya dijitali, hauondoshi ukweli kwamba maudhui yaliyomo kwenye kitabu, ndicho kitu kinachowavuta wasomaji, na sio njia ambayo kitabu hicho kinawasilishwa.

Kwa mujibu wa Rais wa Jumuiya ya Wachapishaji na Wauza Vitabu wa Ujerumani, Gottfried Honnefelder alisema kwamba kati ya Euro bilioni 9.6 zilizoingizwa na sekta ya vitabu mwaka huu, ni asilimia moja tu ambayo imetokana kwa mauzo ya njia ya dijitali. Lakini alisema kwamba, anatarajia kwamba soko hili litakua kufikia asilimia 10 ndani ya kipindi kifupi kijacho.

Katika kuonesha namna tamasha hilo lilivyokusudia kuupa nafasi ulimwengu wa dijitali, mara hii tamasha hili litakuwa na kitengo maalum kinachoitwa "Frankfurt Hot Spots". Mwandishi wa vitabu wa Uingereza, Ken Follett, anatarajiwa kuwasilisha rasimu ya mtandaoni ya kitabu chake maarufu cha The Pillars of he Earth."

Kama kawaida, tamasha hili litashirikisha usomaji wa kitabu, ambapo mara hii mwandishi wa vitabu kutoka Marekani, Jonathan Franzen, atasoma kurasa za kitabu chake "The Freedom" kilichovutia wahakiki wengi duniani. Kazi nyengine zitakazowasilishwa kwenye tamasha hili ni pamoja na zisizo za kifasihi, kama kitabu cha mwimbaji David Bowie "Object" ambacho kina dondoo 100 za maisha yake binafsi.

Mwandishi wa riwaya wa Kiswisi mwenye asili ya Hungary, Melinda Nadj Abonji, ndiye aliyechaguliwa kuwa mwandishi bora wa riwaya kwa mwaka huu kutokana na riwaya yake "Tauben Fliegen Auf" yenye maana ya Njiwa Wanabweruka. Kuchaguliwa kwa mwandishi huyu, ambaye mwenyewe ni mhamiaji wa Kiserbia kutoka Hungary katika tamasha hili ambalo lina mizizi yake kwenye jamii ya Kijerumani, ni dalili za kufunguliwa milango ya muingiliano na mafahamiano baina ya tamaduni.

Nchi iliyopewa heshima ya kuwa mgeni rasmi wa tamasha la mwaka huu ni Argentina, ambayo inasifiwa kwa kutunza utamaduni mkongwe wa usomaji vitabu. Nchi iliyopewa heshima kama hii mwaka jana, ilikuwa ni China, lakini wakosoaji wake walisema kwamba halikuwa jambo zuri kuipa nchi hiyo heshima kubwa kama hii, wakati yenyewe haiheshimu uhuru wa maoni na kujieleza.

Mwandishi: Mohammed Khelef