Taifa jipya liko njiani kuzaliwa Afrika? | Matukio ya Kisiasa | DW | 07.01.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Taifa jipya liko njiani kuzaliwa Afrika?

Watu wa Sudan ya Kusini watapiga kura ya maoni Jumapili ijayo kuamua iwapo watajitenga na Sudan ya Kaskazini, na ishara zote zinaonyesha kwamba Sudan ya Kusini itajitenga tu.

Vifaa vya kupigia kura ya maoni nchini Sudan

Vifaa vya kupigia kura ya maoni nchini Sudan

Maelfu ya watu wanamimika kwenye vituo vya kupigia kura. Baadhi yao wamesafiri kwa muda wa wiki tatu, kwa magari na mitumbwi ili kuwahi siku ya kupiga kura. Mongoni mwa waliowasili kutoka Sudan ya Kaskazini ni Angelo Loki, ambaye anasema kwamba waliambiwa na baadhi ya watu Sudan ya Kaskazini kwamba, kama Sudan ya Kusini itajitenga, maisha yao katika Sudan ya Kaskazini yangelizidi kuwa magumu.

"Serikali ya Sudan ya Kusini imetuambia kwamba sasa tunaweza kurejea nyumbani. Na ndiyo sababu nimeamua kuwa njiani kurejea nyumbani." Anasema Loki.

Halikuwa jambo rahisi kwa Loki, ambaye sasa ana umri wa miaka 55 kuamua njia hiyo. Aliishi katika mji wa Khartoum tokea utoto wake. Amekulia katika mji huo ambapo pia alienda shule. Loki ana mke anayetoka Sudan ya Kaskazini aliyezaa naye watoto watano. Amekuwa anafanya kazi ya ufundi wa magari yenye kipato kizuri.

Matayarisho ya upigaji wa kura ya maoni Sudan ya Kusini

Matayarisho ya upigaji wa kura ya maoni Sudan ya Kusini

Lakini kutokana na mazingira ya kisiasa, amelazimika kuondoka Khartoum bila ya mke na watoto wake. Alisafiri kwa mashua kutoka Kaskazini. Kutokana na gharama za safari hakuwa na fedha za kutosha ili kuichukua familia yake yote. Safari ya kurudi nyumbani Sudan ya kusini imemgharimu akiba yake yote ya fedha.

Hata hivyo, Loki anatumai kwamba watoto wake watakuwa na maisha mazuri katika Sudan ya Kusini, ikiwa watu wa sehemu hiyo wataamua kujitenga hapo Jumapili.

Kwake Loki mambo yote ni wazi kabisa. Anataka Sudan ya Kusini ijitenge.

"Mimi nataka uhuru. Nimeviona vita vililivyoikumbanchi yetu. Waarabu wametufanyia mambo mabaya sisi watu wa kusini. Wamekiuka haki na ubinadamu wetu. Natumai mke na watoto wangu watakuja kuishi Kusini baada ya kura ya maoni." Anasema Loki.

Kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyochukua muda wa miaka 20,Sudan imekuwa nchi yenye idadi kubwa ya wakimbizi, kuliko nyingine yoyote duniani. Kwa mujibu wa takwimu, wapo wakimbizi milioni nne wa Sudan waliotawanyika katika nchi za jirani,Ulaya, Marekani na Canada. Wengine wamefika hadi Australia. Na kwa mujibu wa hesabu za Umoja wa Mataifa WaSudan kusini milioni 1 na nusu wanaishi kaskazini. Maalfu sasa wanarejea kila siku. Umoja wa Mataifa unashirikiana na serikali ya Sudan ya Kusini katika kuwasaidia watu hao.

Mwandishi: Simone Schlindwein/ZR

Tafsiri: Mtullya, Abdu

Mhariri: Miraji Othman

DW inapendekeza

 • Tarehe 07.01.2011
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/zusg
 • Tarehe 07.01.2011
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/zusg

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com