Syria yahanikiza magazetini | Magazetini | DW | 30.05.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Syria yahanikiza magazetini

Na kama ada yetu ya kila siku tunakuletea baadhi ya yale waliyoyaandika wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo katika safu zao za maoni.

Rais wa Syria Bashar al Assad

Rais wa Syria Bashar al Assad

Na leo wahariri hao wanauzungumzia mgogoro wa Syria na ziara ya Rais wa Ujerumani Joachim Gauck nchini Israel.

Juu ya mgogoro wa Syria gazeti la "Wiesbadener Kurier" linasema:

Kujiingiza kijeshi nchini humo kutokea nje, licha ya mauaji yanayoendelea, ni vigumu kufikiria. Kwa sababu madhara yake katika eneo zima linalopakana na nchi hiyo hayawezi kupimika.

Mhariri wa gazeti la"Wiesbadener Kurier" anaendelea kwa kusema:

Tajiriba ya nchini Libya imeonyesha kuwa anaeumwa na nyoka hushtushwa na ukoka.Pana hofu kwamba baada ya kujiingiza kijeshi na kumtoa Assad, wapinzani watakaoshinda watatoa mwito wa kuunda serikali ya waislamu wenye itikadi kali na hivyo kuyahatarisha mapinduzi katika nchi nyingine za kiarabu.Kutokana na hali hiyo, matumaini bado yapo katika mpango wa amani wa Kofi Annan.

Lakini mhariri wa gazeti la "Südwest Presse" ana mtazamo tofauti na anasema:

Kutokana na watawala kuwaua watu wananchi wao wenyewe , pamoja na watoto,sasa hakuna kurudi nyuma tena katika juhudi za kidiplomasia. Kwa hivyo ni sahihi kabisa kwa Ujerumani kuchukua hatua ya kumtimua balozi wa Assad nchini Ujerumani.

Ilikuwa dhihaka ya kiasi gani kwa polisi wa Ujerumani kumlinda balozi wa Syria mjini Berlin wakati utawala wake nyumbani unawaua raia.

Gazeti la "Der Tagesspiegel" linasema sasa wakati umefika kwa jumuiya ya kimataifa kujiuliza iwapo, itakuwa sahihi kuendelea kuuchochea moto wa vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa kuwapa silaha wapinzani.Gazeti hilo linaeleza:

Rais wa Ujerumani Joachim Gauck

Rais wa Ujerumani Joachim Gauck

Urusi na Iran zinaupa silaha utawala wa Assad wakati,nchi za Ghuba na yumkini Marekani zinawaunga mkono wapinzani kijeshi.Katika hali hiyo vita vya kiwakala vinapamba moto mithili ya vile tulivyoviona katika enzi za vita baridi.

Rais wa Ujerumani Joachim Gauck anaendelea na ziara rasmi nchini Israel. Wahariri pia wanatoa maoni juu ya ziara hiyo.

Gazeti la "Nordwest Zeitung" linasema:

Ziara ya Rais Gauck nchini Israel siyo hatua rahisi, kwani pia atautembelea Ukingo wa Magharibi.Gauck kama rafiki wa dhati wa Israel hatauficha msimamo wake. Lakini katika wasaa mzuri atapaswa kuwaambia rafiki zake -kuwa kuhusu mambo fulani pana haja ya kutumia neno hapana.

Na gazeti la "Der neue Tag" linatilia maanani kwamba ,kwa wanasiasa wa Ujerumani ziara za nchini Israel , wakati wote ni suala nyeti.Wanapaswa kutumia maneno sahihi kwenye mazungumzo. Linaandika

Lakini mpaka sasa Rais Gauck ameuonyesha uwezo huo.Ametumia sauti mwafaka.Hayo ni muhimu hasa katika muktadha wa shairi la mwandishi maarufu wa Ujerumani, Günter Grass na pia kutokana na matokeo ya kura ya maoni ya hivi karibuni iliyoonyesha kwamba hadhi ya Israel miongoni mwa wananchi wa Ujerumani imepungua.

Mwandishi: Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman