Syria: Mbinyo wazidi kwa Urusi na China
6 Juni 2012Urusi imo katika mbinyo unaoongezeka ili kuunga mkono kuondoka kwa Bashar al-Assad madarakani kama hatua ya mwanzo katika makubaliano ya amani ambayo yatasabasha watu wa karibu na Assad kuchukua madaraka ya mpito, chini ya makubaliano kama yaliyopatikana nchini Yemen na kuungwa mkono na umoja wa mataifa ya serikali ya mpito nchini Yemen mwaka huu.
Naibu waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Gennady Gatilov amesema , " Hatujawahi kusema ama kusisitiza kuwa ni lazima Assad abaki madarakani ifikapo mwishoni mwa utaratibu wa kisiasa",
Suala hili ni lazima lisuluhishwe na Wasyria wenyewe, ameongeza naibu waziri huyo akinukuliwa na shirika la habari la Urusi ITAR-TASS.
Taarifa hiyo ni moja kati ya taarifa za wazi kabisa za Urusi juu ya nafasi ya Assad tangu waziri wa mambo ya kigeni wa nchi hiyo Sergei Lavrov kukataa wazi kuunga mkono utawala wa Assad wakati alipofanya ziara nchini Syria Februari mwaka huu.
Urusi yakata mkutano wa kimataifa
Wakati huo huo waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov ametoa wito leo wa kuitishwa mkutano wa kimataifa kuhusu mzozo wa Syria utakaojumuisha mataifa ya Iran na Uturuki kwa lengo la kuunga mkono mpango unalega lega wa amani uliofikiwa kwa upatanishi wa mjumbe wa kimataifa Kofi Annan.
Taarifa hiyo imekuja wakati Urusi na China , ambazo zimezuwia hatua zinazoongozwa na mataifa ya magharibi dhidi ya Syria, kuanza mazungumzo yanayohusu kufikisha mwisho karibu miezi 15 ya ghasia ambazo zimesababisha watu zaidi ya 13,500 nchini Syria kuuwawa na karibu watu wengine 47 wamepoteza maisha jana Jumanne.
Marekani yataka ushirikiano zaidi
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Hillary Clinton amezitaka China na Urusi kuwa sehemu ya suluhisho la mzozo wa Syria baada ya kukubaliana kufanyakazi kwa karibu zaidi katika umoja wa mataifa.
Balozi wa China katika umoja wa mataifa Li Baodong amesema kuwa juhudi za kumaliza mauaji zimeingia utata na kwamba majeshi ya serikali na waasi ni lazima yasitishe mapigano. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya China Liu Weimin amesema.
"China na Urusi sinapinga vikali mataifa ya kigeni kuingilia kati nchini Syria na zinapinga mabadiliko ya utawala kwa kutumia nguvu".
Kuongezeka kwa matumizi ya nguvu na ghasia nchini Syria kumesababisha mataifa ya Kiarabu kuelezea wasi wasi wao juu ya uwezekano wa mpango wa amani wa umoja wa mataifa , ambao umefikiwa kwa upatanishi wa mjumbe wa kimataifa Kofi Annan.
Waziri mkuu mpya Syria
Wakati huo huo rais Bashar al-Assad amemteua waziri wa zamani wa kilimo nchini humo na ambaye ni mshirika wake wa karibu Riyad Hijab kuwa waziri mkuu mpya. Anachukua nafasi inayoachwa wazi na Adel Safar ambaye aliteuliwa kushika wadhifa huo Aprili mwaka jana.
Mwandishi : Sekione Kitojo /dpae / ape/ afpe
Mhariri: Moahammed Abdul-Rahman