Sudan ya Kusini kutangazwa taifa huru
31 Januari 2011Rais Salva Kiir wa eneo hilo la kusini lenye utawala wa ndani akitangaza habari hiyo, aliongezea kuwa Juba huenda ukawa mji mkuu wa taifa hilo jipya, litakalokuwa taifa la 54 barani Afrika na 193 duniani.
Kwa mujibu wa halmashauri ya uchaguzi, takriban asilimia 99 ya wapiga kura wa Sudan ya Kusini, walioshiriki katika zoezi la kura ya maoni, mwanzoni mwa mwezi huu, wameamua kujitenga na kaskazini. Maelfu ya watu walisherehekea matokeo hayo mjini Juba.
Mapema mwezi huu, Rais wa Sudan Omar al-Bashir alisema kuwa atatambua matokeo ya kura hiyo ya maoni ambayo ni sehemu ya makubaliano ya amani ya mwaka 2005. Makubaliano hayo yalimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu miaka 22 nchini humo na kusababisha vifo vya zaidi ya watu milioni mbili na mamilioni wengine kupoteza makaazi yao.