Sri Lanka yasherehekea miaka 60 ya uhuru | Matukio ya Kisiasa | DW | 04.02.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Sri Lanka yasherehekea miaka 60 ya uhuru

Downtown city street, Colombo, Sri Lanka, video still

Mji mkuu wa Sri Lanka Colombo upo chini ya ulinzi mkali

Sri Lanka leo inasherehekea mwaka wa 60 tangu kupata uhuru wake kutoka Uingereza katika mwaka 1948.Sherehe rasmi zimefanywa chini ya ulinzi mkali katika juhudi ya kuzuia wimbi la mashambulizi ya waasi wa Tamil Tigers.

Rais wa Sri Lanka Mahinda Rajapakse alifungua sherehe rasmi za kuadhimisha miaka 60 ya uhuru wa kisiwa hicho akiwa chini ya ulinzi mkali kabisa.Maafisa wa usalama wamesema,miongoni mwa hatua pekee zilizochukuliwa ni kuzuia kwa muda upelekaji wa habari fupi kwa simu za mkono yaani SMS.Huduma zilisitishwa kuanzia leo asubuhi hadi mchana zilipomalizika sherehe rasmi zilizofanywa mbele ya pwani mjini Colombo.

Vikosi vya usalama vimeuzingira mji mkuu Colombo kufuatia shambulizi la siku ya Jumapili.Katika shambulizi hilo kwenye kituo kikuu cha treni mjini Colombo,muasi wa kike wa Kitamil aliejitolea maisha muhanga aliripua bomu na kusababisha vifo vya watu 13.Zaidi ya 100 wengine walijeruhiwa katika shambulizi hilo la bomu.

Rais Rajapakse katika hotuba yake kwa taifa,ameapa kuimarisha jitahada za kukomesha ugaidi na amesema, maeneo yanayodhibitiwa na waasi wa Kitamil kaskazini mwa nchi yatakombolewa.Akaongezea kuwa waasi wa Tamil Tigers wanapigwa vibaya na majeshi ya serikali katika duru mpya ya mapigano,huku mgogoro wa kikabila ukiendelea kwa takriban miongo mitatu.

Rajapakse aliechaguliwa rais miaka miwili iliyopita,amesema kuwa katika kipindi hicho,vikosi vya serikali vimefanikiwa kukomboa mkoa wa mashariki na sasa,waasi wamebaki katika wilaya mbili,kaskazini mwa nchi.

Lakini waasi wa Kitamil sasa wameimarisha mashambulizi yao kusini mwa nchi wakitumai kuwa vikosi vya serikali vitaondoshwa kaskazini mwa nchi na kupelekwa kwenye maeneo ya mapigano mapya.Kwani hivi karibuni,majeshi ya serikali yalianzisha operesheni kali za kijeshi katika eneo hilo la kaskazini lililo katika mikono ya waasi.

Zaidi ya raia 100 wameuawa tangu serikali hapo tarehe 16 Januari kujitoa kwenye mkataba wa amani uliotiwa saini pamoja na Tamil Tigers miaka sita iliyopita.Chama cha Tamil Tigers cha LTTE kinagombea uhuru wa eneo la kaskazini na mashariki mwa Sri Lanka, kwa ajili ya Watamil.Sri Lanka ni nchi yenye wakaazi wengi zaidi wa kabila la Sinhala.

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com