1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SPLM kugombania urais wa Sudan

Kalyango Siraj28 Julai 2008

Haya ni mafanikio ya mkataba wa amani wa 2005

https://p.dw.com/p/ElNN
Kiongozi wa SPLM, Salva Kiir Mayardit (Kushoto) akizungumza na rais wa Sudan Omar al-Bashir (Kulia)Picha: picture-alliance/dpa/dpaweb

Kiongozi wa zamani wa waasi wa kusini mwa Sudan Salva Kiir atagombania urais wa Sudan katika uchaguzi ujao.Hii ni kwa mujibu wa maafisa wa chama chake cha Sudan People's Liberation Movement SPLM.

Taarifa za kuwa makamu rais wa Sudan na wakati huohuo rais wa Sudan Kusini Salva Kiir kugombania kiti cha rais wa Sudan moja katika uchaguzi ujao zimetolewa na maafisa wa chama chake cha SPLM.

Ikiwa kweli atashiriki katika uchaguzi uliopangwa kufanyika mwaka ujao, hii itakuwa moja wa mfanikio ya mkataba wa amani wa mwaka 2005 ambao ulikomesha vita vya ndani vya mda mrefu ambavyo ndivyo vilivyochukua mda mrefu kuliko vyote vya aina hiyo barani Afrika.

Vita vilikuwa kati ya waarabu wa kaskzini na weusi wa kusini.

Vita hivyo vilianza mwaka wa 1983 hadi 2005.Lakini wataalamu wanasema kuwa hivyo vilikuwa sehemu ya pili ya vile vilivyotangulia vya mwaka wa 1955 hadi 1972.

Mgogoro huo ulimalizika rasmi mwaka wa 2005 wakati uliposainiwa mkataba wa amani januari ya mwaka huo.

Pande mbili husika zilikubaliana kugawana madara, utajiri,na kuweka eneo la kusini linalojitawala lenyewe na kuahidi kufanyika uchaguzi uliohuru na wa haki nchini kote na pia kufanyika kwa kura ya maoni mwaka wa 2011sehemu za kusini za nchi hiyo kuamua ikiwa kweli raia wa huko wanataka kujitenga.

Kutokana na mkataba huo wa amani, chama cha waasi wa kusini cha SPLM kilijiunga na serikali ya Khartoum na kiongozi wake Salva Kiir kuteuliwa kuwa makamu wa kwanza wa rais wa Sudan yote.

Kuhusu kiongozi wao kugombania urais katika uchaguzi ujao, afisa wa ngazi za juu wa chama hicho,Yasir Arman ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa chama chao kimeamua rasmi kuwa kitagombania nafasi zote katika uchaguzi ujao.

Uamuzi huo ,ameongeza kuwa,umefikiwa baada ya mkutano wa viongozi wa chama wa ngazi zote uliochukua siku kadhaa.

Hakusema ulikaa wapi,bali alisema kuwa kiongozi wao Salva Kiir atateuliwa kugombania urais akiongeza kuwa, ishara zote zaonyesha kama chama cha SPLM kina nguvu na bila shaka kitapata ushindi .

SPLM kina wanachama maelfu kadhaa ,waliosajiliwa rasmi katika sehemu za kaskazini,lakini baadhi wanasema kuwa kiongozi wao Salva Kiir hakai sana Khartoum.Wanaongeza kuwa hata mawaziri wengi wa SPLM walioko katika serikali kuu hawajishughulishi ipasavyo.

Mbali na yote hayo kizingiti muhimu katika mkataba huo wa amani ni eneo la katikati linalogombaniwa la Abyei.Eneo hilo linautajiri wa mafuta.Nalo litapiga kura ya maoni mwaka wa 2011 kuhusu kujitenga kutoka kwa utawala wa Khartoum.

Jana jumapili jeshi la kaskazini limehakikisha kuwa limeondoa kabisa vikosi vyake kulingana na mkataba huo amani na kuacha kikosi cha jeshi la pamoja .

Kuhusu mgogoro wa sasa nchini humo afisa huyo amesema kuwa maaafisa wa chama chake hivi karibuni watakaa na wenzao wa chama cha rais Bashir cha National Congress Party NCP kujadilia jinsi ya kuweza kuutanzua mgogoro huo.