1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SPD yaunga mkono mazungumzo na Merkel

Sekione Kitojo
21 Januari 2018

Chama cha  Social Democratic SPD kimepiga  kura kuunga  mkono  kuanza  kwa mazungumzo  ya  mwanzo  ya  kuunda  serikali  ya  mseto na  chama  cha kansela Angela Merkel.

https://p.dw.com/p/2rGD3
Außerordentlicher SPD-Parteitag Abstimmung über Große Koalition
Wajumbe wa SPD wakipiga kura kuunga mkono mazungumzo na chama cha MerkelPicha: picture alliance/dpa/K. Nietfeld

Hatua  hiyo  imeliingiza  taifa  hilo  ambalo  ni  uchumi  mkubwa  katika  bara  la Ulaya  hatua  moja  karibu  na   kupata  serikali  imara  baada  ya miezi  kadhaa ya  hali  ya sintofahamu  ya  kisiasa.

Wajumbe  wa  chama  cha  SPD walipiga  kura  362 za  'ndio'  dhidi  ya  kura  279  za 'hapana" kusongambele  na  majadiliano  baada  ya  viongozi  wa  chama  hicho  cha  siasa za  wastani  zan  mrengo  wa  kushoto  kukubali  muongozo wa  muungano  pamoja  na  kundi la  vyama  vya  kihafidhina  vinavyoongowa  na  kansela  Merkel  mapema  mwezi  huu. Hakuna  mjumbe  aliyejizuwia  kupiga  kura.

Außerordentlicher SPD-Parteitag SPD-Parteivorsitzender Martin Schulz
Kiongozi wa chama cha SPD Martin SchulzPicha: picture alliance / Federico Gambarini/dpa

Mazungumzo  yanatarajiwa  kuanza  wiki  hii, na  kuleta ahueni  kwa  washirika  wa  Ujerumani barani  Ulaya , ambako  Merkel  kwa  muda  mrefu  amechukua  nafasi  ya  uongozi  katika masuala  ya  kiuchumi  na  usalama. Wajumbe  wa  chama  cha  SPD  bado  watakuwa  na nafasi  ya  kupiga  kura  katika  makubaliano  ya  mwisho  ya  kuunda  serikali , kama yatapatikana.

Kiongozi  wa  chama  cha  Social Democratic SPD Martin Schultz  hapo  awali  katika hotuba  yake  kwa  wajumbe aliwataka wanachama wa chama  hicho kupiga kura kwa  ajili ya  kufungua  mazungumzo  ya  kuunda  serikali ya  mseto na  chama  cha  kansela  Merkel, akisema  serikali  imara  ya  Ujerumani  inahitajika  kuimarisha  Ulaya  na  kuwa kama  ukuta dhidi  ya  siasa  kali za  mrengo wa  kulia.

Außerordentlicher SPD-Parteitaga Abstimmung
Mkutano wa chama cha SPD mjini BonnPicha: Reuters/W. Rattay

Uamuzi wake ulikuwa sahihi

Chama  hicho  cha  siasa za wastani  za  mrengo  wa  kushoto  kimeshiriki  katika  serikali na  kundi  la  vyama  vya  kihafidhina  la  kansela  Angela  Merkel  tangu  mwaka  2013, lakini Schultz aliapa  kutorejea  tena  katika  kile  kinachoitwa "muungano  mkuu" baada  ya  chama chake  cha  Social Democratic kupata  kipigo  katika  uchaguzi  wa  mwezi  Septemba.

Amewaambia  wanachama  wa  chama  chake  waliokusanyika  mjini  Bonn kwamba  uamuzi wake ulikuwa  sahihi katika  wakati  ule, lakini  alisema  hali  ya  kisiasa  imebadilika  baada ya  Merkel  kushindwa  kuunda  serikali pamoja na  vyama  viwili vidogo.

"Ulaya  inaisubiri  Ujerumani  ambayo  inafahamu  wajibu  wake kwa  ajili  ya  Umoja  wa Ulaya   na  inaweza  kuchukua  hatua muafaka," alisema.

Amesema  hali  ni  ngumu, wakati  rais  wa  Ufaransa Emmanuel Macron  anahitaji  kuungwa mkono  kwa  mipango  yake  ya  kuufanyia  mageuzi Umoja  wa  Ulaya.

"Iwapo atashindwa  katika  sera  zake , haitawezekna  kuondoa uwezekano  wa  makundi yenye  siasa  kali  za  mrengo  wa  kulia  kuunda  serikali ijayo  mjini  Paris," Schutz  alisema.

Außerordentlicher SPD-Parteitag Andrea Nahles und Martin Schulz
Mkuu wa kundi la wabunge wa SPD bungeni Andrea nahles na kiongozi wa SPD Martin SchulzPicha: picture alliance/dpa/K. Nietfeld

Iwapo  Wasocial Democrats  watakataa  kuingia  katika  mazungumzo , fursa  pekee iliyokuwa imebaki  ni  kwa  Merkel  kuunda  serikali yenye  wingi  mdogo  ama  kuitisha uchaguzi  mpya.

Naibu  kiongozi  wa  chama  cha  Social Democratic  Malu Dreyer , gavana  wa  jimbo  la Rhineland-Palatinate, aliwaambia  wajumbe  wa  mkutano  huo  kwamba  kwa  kuwa   kundi la  vyama  vinavyoongozwa  na  Merkel  linapinga  kuunda  serikali  yenye  wingi  mdogo , kupiga  kura  dhidi  ya  kuingia  katika  mazungumzo hayo kutakuwa  na  maana ya kufanyika uchaguzi  mpya.

Vijana  wanapinga  makubaliano hayo

"Hatuwezi  kuvilazimisha  vyama  vya  kihafidhina  kuunda  serikali  ya  wingi  mdogo, hii  ni kitu  ambacho  hakipo," alisema.

Lakini  kiongozi wa  tawi  la  vijana  la  chama  cha  Social Democratic , Kevin Kuehnert, aliwahimiza wajumbe  kupiga  kura  dhidi  ya  kuingia  katika  muungano  huo wa  serikali, akisema  kukubali  kwa  sababu  tu  ndio  njia pekee  iliyobakia  kutachangia  zaidi  katika matatizo  makubwa  ya  chama  hicho ya  kutoaminika  na  waungaji  wake  mkono.

"Mzunguko  huu  ni  lazima  uvunjwe,"  amesema  Kuehnert , ambaye  aliongoza  upinzani mkali  dhidi  ya  kuingia  katika  mazungumzo  mapya  ya  kuunda  serikali  ya  muungano.

Wengi  wa  wanachama  wa  chama  cha  Social Democratic  wameeleza  hofu  yao kwamba watakapoingia  katika  muungano wa  serikali  mpya , hii  itakiweka  chama  kinachopinga wahamiaji  cha  Alternative for Germany , chama  mbadala  kwa  Ujerumani AfD kuwa  chama kikuu  cha  upinzani  bungeni.

Außerordentlicher SPD-Parteitag nogroko
Kampeni ya kupinga serikali ya mseto na chama cha CDU katika mkutano wa chama cha SPD , "NOGROKO"Picha: picture alliance/AP/M. Probst

Lakini  Schulz amesema  kitisho  cha  uchaguzi  mpya  ni  kikubwa  zaidi. "Nani  anaweza kusema  kwamba  uchaguzi  mpya  hautaimarisha  zaidi  kundi  la  siasa  kali  za  mrengo  wa kulia?"  aliuliza.

Alidokeza  kwamba  Wa Social Democrats wengine  barani  Ulaya hawajafidika na  kuwa katika  nafasi  hiyo,  na  kueleza  kwamba  nafasi  nzuri  kwa  chama  chake  kupata  kuungwa mkono  zaidi  kutoka  mashinani ni  kupitia  kuendeleza  kwa  nguvu  zote  sera  zake  kutokea ndani  ya  serikali  na  kuchukua  hatua  kama  chama  mshirika  mdogo  na  Merkel.

"Serikali  yoyote ambacho  chama  cha  SPD  kitashiriki , bila  kujali  ni  muungano   gani, inapaswa  kuwa  serikali  ya  SPD," alisema. "Huo ni  lazima  uwe msimamo  wetu."

Mwandishi : Sekione Kitojo / ape

Mhariri: Isacc Gamba