1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Somalia: Pande zinazopigana zajiwinda tena kwa mapambano.

Serikali dhaifu ya Somalia imewalaumu kundi la al-Qaida nchini humo kwa jaribio lililoshindwa la kumuua kamanda wake mkuu wa jeshi la Somalia, na kisha kuwataka raia walioko katika maeneo yanayoshikiliwa na waasi kuondoka katika majumba yao kabla ya kufanyika shambulio kubwa la kijeshi.

Majeruhi katika vita nchini Somalia wakiwa hospilini.

Majeruhi katika vita nchini Somalia wakiwa hospilini.

Wakati umoja wa mataifa pamoja na mashirika ya kutoa msaada wakionya kuwa mamia kwa maelfu ya watu wanakimbia mapigano makali kabisa kuwahi kuonekana mjini Mogadishu katika muda wa miaka 15 ya machafuko nchini humo, hofu inazidi kutanda kuwa hali ya kusita mapigano kwa muda wa siku nne sasa inakaribia kufikia mwisho.

Naibu waziri wa ulinzi Salad Ali Jelle amesema kuwa serikali yake haitambui makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa jana Jumapili baina ya majeshi ya Ethiopia na wazee wa kiukoo , wakati majeshi ya Ethiopia yalikuwa yakionekana yakijiweka katika nafasi karibu na ngome za wanamgambo hao wa mahakama za Kiislamu.

Wakati huo huo , Jenerali Abdullahi Ali Omar, kamanda wa jeshi la Somalia , alinusurika kuuwawa katika shambulio la bomu lililotegwa kando ya barabara wakati akisafiri katika mlolongo wa magari ya serikali kutoka katika hoteli anakoishi leo asubuhi.

Mwanajeshi mmoja amejeruhiwa katika mlipuko huo, amesema msemaji wa rais nchini Somalia Hussein Mohammed Hussein.

Licha ya kuwa mapigano yamepungua makali leo Jumatatu , majeshi ya Ethiopia yaliwapiga risasi na kuwauwa raia wanne , kwa mujibu wa watu walioshuhudia , na wengi wanaendelea kukimbia , wakieleza kuwapo na uhaba mkubwa wa chakula na maji.

Miili kadha ya watu ikiwa inaoza imetapakaa katika mitaa, na nyumba nyingi ni tupu.

Shirika la umoja wa mataifa la kuwahudumia wakimbizi limesema kuwa watu karibu 10,000 wamekimbia kutoka mji mkuu wa Mogadishu katika muda wa siku tatu zilizopita , na kufikisha idadi jumla ya watu ambao wamekimbia makaazi yao kufikia 100,000 tangu mwezi Februari.

Wakati huo huo rais wa Eritrea Issaias Afeworki amekutana na rais wa Uganda Yoweri Museveni katika mji wa bandari nchini humo wa Massawa ili kutafuta njia muafaka ya kurejesha utulivu mjini Mogadishu, maafisa wamesema.

Hasimu mkuu wa Ethiopia, Eritrea imeishauri Uganda kuondoa majeshi yake ya kulinda amani kutoka Somalia , wakionya kutokea madhara makubwa iwapo majeshi hayo yaliyopelekwa hivi karibuni yatabakia huko.

Wachunguzi wa masuala ya kisiasa wanaeleza wasi wasi wao kuwa Ethiopia na Eritrea, ambazo bado zinavutana kuhusiana na mzozo wa mwaka 1998-2000 wa mpaka, huenda wakapigana vita ya kupimana nguvu.

 • Tarehe 02.04.2007
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CB4x
 • Tarehe 02.04.2007
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CB4x

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com