Siri za majadiliano ya Mashariki ya Kati nje nje
24 Januari 2011Inasemekana kuwa hati hizo ni kutoka majadiliano yaliyofanywa mwaka 2008, kati ya mawaziri wa nje wa wakati huo, Condoleezza Rice wa Marekani, Tzipi Livni wa Israel, waziri mkuu wa zamani wa Wapalestina Ahmad Qorei na mpatanishi mkuu wa Wapalestina Saeb Erekat.
Al Jazeera imesema kuwa imepata zaidi ya hati 1,600 za siri zinazohusika na majadiliano ya amani ya Mashariki ya Kati yaliyofanywa kati ya Israel na Wapalestina. Kuambatana na hati hizo, mpatanishi mwandalizi wa Kipalestina, wakati huo alipendekeza kuwa Israel ibakie na makaazi yote ya walowezi wa Kiyahudi katika mji wa Jerusalem, isipokuwa eneo moja lililojengwa baada ya Israel kuivamia Jerusalem ya Mashariki mwaka 1967.
Wiki iliyopita tu, Rais wa Wapalestina Mahmoud Abbas alisema kuwa Jerusalem ni yao na hilo wala si suala la kujadiliwa. Mpatanishi mkuu wa Wapalestina, Saeb Erekat alipohijiwa na Al Jazeera alisema, serikali ya Wapalestina haina cho chote cha kuficha na ameipuza ripoti hiyo kama ni uwongo mtupu. Kwa sasa, majadiliano ya amani yamekwama. Wapalestina wanakataa kurejea kwenye meza ya mazungumzo mpaka Israel itakapositisha ujenzi wa makaazi ya Wayahudi katika maeneo ya Waarabu.