1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku ya kupinga ubaguzi duniani

Sylvia Mwehozi
21 Machi 2017

Tarehe 21 Machi ni siku ya kimataifa ya kupinga ubaguzi duniani ambapo kauli mbiu ya mwaka huu 2017 ni vitendo vya ubaguzi wa rangi na uchochezi wa chuki katika muktadha wa uhamiaji.

https://p.dw.com/p/2ZeUU
Mittelmeer - Flüchtlinge – Boot
Picha: Getty Images/AFP/A. Messinis

Kila binadamu anayo haki ya kupata haki za binadamu bila ya ubaguzi. Haki za usawa na kutobaguliwa ni suala muhimu katika sheria za haki za binadamu. Hata hivyo katika maeneo mengi ya dunia , vitendo vya ubaguzi bado vimeenea, ikiwemo ubaguzi wa rangi, makabila, dini, utaifa na uchochezi wa chuki.

Kuwabagua watu kwa misingi ya rangi na makabila kunaelezwa kama "utegemezi wa utekelezaji wa sheria, ulinzi na udhibiti wa mtu katika mipaka kwa kuzingatia rangi, ukabila, asili ya taifa au ukabila kama misingi ya  kuwaingiza watu na utafutaji wa kina, utambulisho na uchunguzi, au kwa ajili ya kuamua iwapo mtu fulani anashiriki  katika shughuli za uhalifu,", hiyo ni kulingana na ripoti ya hivi karibuni ya Baraza la Haki za Binadamu na mwandishi maalum juu ya aina ya ubaguzi wa rangi wa kisasa, na ubaguzi unaohusiana na chuki dhidi ya wageni.

Kopie eines italienischen Passes
Mwanaume akionyesha nakala ya mbele ya pasipoti ya Italia wakati wa mkutano dhidi ya ubaguzi Bolgona, ItaliaPicha: picture-alliance/dpa/G. Benvenuti

Wakimbizi pamoja na wahamiaji ndio haswa walengwa katika ubaguzi wa rangi na uchochezi wa chuki. Katika azimio la wakimbizi na wahamiaji la jijini New York lililopitishwa mwezi Septemba mwaka jana, wanachama wa Umoja wa Mataifa walikemea vikali vitendo na dalili za ubaguzi, ubaguzi wa rangi , chuki dhidi ya wageni na vitendo vingine vinavyohusiana na hayo kwa wakimbizi na wahamiaji na kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na mitazamo na tabia kama hizo hasa kuhusu uhalifu wa chuki, kauli za kichochezi na vurugu za kibaguzi.

Mkutano wa kilele wa wakimbizi na wahamiaji wa mwezi Septemba mwaka jana pia ulikuja na kampeni ya "pamoja" , ikiwa ni hatua ya Umoja wa Mataifa ya kuhamasisha heshima, usalama na utu kwa wakimbizi na wahamiaji.  Kampeni hiyo ni ya kidunia ikiongozwa na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa inayolenga kubadili fikra hasi na mitazamo hasi dhidi ya kundi hilo, kwa kushirikiana na nchi wanachama, asasi za kiraia na sekta binafsi.

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imewataka watu duniani kusimama na kutetea haki za watu hii leo. Kampeni hii iliyozinduliwa siku ya haki za binadamu  mwaka 2016 inalenga kuhamasisha na kuunga mkono matendo ya kila siku katika maisha ya mwanadamu ya kutetea haki za binadamu kwa ajili ya wengine. Popote tulipo, tunaweza kuleta mabadiliko, kwasabababu inaanza na sisi sote. Je ni kwa namna gani wewe unatetea haki za binadamu?

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/http://www.un.org/en/events/racialdiscriminationday/

Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman