Siasa za Ufaransa zatikiswa na kesi ya ubakaji dhidi ya Strauss-Kahn | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.05.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Siasa za Ufaransa zatikiswa na kesi ya ubakaji dhidi ya Strauss-Kahn

Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Fedha, IMF, Dominique Strauss-Kahn, anatarajiwa kufikishwa mahakamani hii leo jijini New York kujibu mashtaka ya jaribio la kumbaka mhudumu wa hoteli jijini humo.

default

Dominique Strauss-Kahn, akisindikizwa nje ya kituo cha polisi New York

Tukio hili limekuja wakati Strauss-Kahn akiongoza kampeni ya shirika lake kuyasaidia mataifa yanayotumia sarafu ya Euro kujikwamua kifedha na wiki chache tu kabla hajatangaza azma ya kuwania urais wa Ufaransa katika uchaguzi ujao.

Akiwa amefungwa pingu na akisindikizwa na maafisa wawili wa idara ya upelelezi ya New York, Mkuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, Dominique Strauss-Kahn alionekana na uso wenye fadhaa usiku wa jana, ikiwa ni mara ya kwanza kuonekana tangu shutuma za ubakaji dhidi yake zitajwe.

Wakili wake, William Taylor, amesema kwamba mteja wake alikubali kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu kwa hiyari yake, na kwamba atayakana mashitaka yote mahakamani hivi leo. Strauss-Kahn anashitakiwa kwa makosa matatu: jaribio la kubaka, shambulio la aibu na kumfungia mtu ndani bila ya ridhaa yake. Kama atatiwa hatiani, mashitaka haya yanaweza kumpeleka jela kwa kipindi kisichopungua miaka 15.

Minong'ono imeanza kuzagaa kwamba kesi hii dhidi ya Meneja Mkurugenzi huyo wa IMF ni mtego wa kisiasa kutoka ndani ya taasisi yake ya IMF na pia kutoka kwa washindani wake nchini Ufaransa, ambako anaonekana kuwa na nafasi nzuri zaidi ya kushindana na rais wa sasa, Nicolas Sarkozy, kwenye uchaguzi wa mwakani.

Lakini polisi jijini New York inasema hakuna siasa yoyote, bali ni suala la kawaida la kisheria. Mapema polisi hiyo ilisema kwamba, mhudumu huyo wa kike alimtaja Strauss-Kahn kuwa ndiye aliyetaka kumbaka kwenye chumba chake kwenye hoteli ya Sofitel, wakati alipooneshwa kumtambua miongoni mwa wanaume wengine watano. Vyombo vya habari vya Marekani vimemnukuu mwanamke huyo akisema kwamba, aliingia chumbani kwa Strauss-Kahn, akidhani hamukuwa na mtu.

Nchini Ufaransa, ambako nyota ya kisiasa ya Strauss-Kahn ndiyo imeanza kung'ara, kumekuwa na wasiwasi kwamba huu ndio mwanzo wa mwisho wake. Dominique Paille wa chama kinachofuata siasa kali za mrengo wa kati, amesema kwa taifa la Ufaransa, hili ni tukio litakalochukuwa muda kusahaulika.

Hata hivyo, serikali ya Rais Sarkozy imeonya kwamba bado ni mapema mno kumuhukumu Strauss-Kahn, licha ya kwamba kesi hii sasa inaipa serikali hiyo fursa nzuri zaidi kwenye uchaguzi wa mwakani.

Naye kiongozi wa chama cha National Front, Marine Le Pen, anayependa kujijenga kama mwanamke anayepambana na dunia ya wanaume kwenye siasa, amesema kwamba kashfa hii haimshangazi sana. Katika kura za maoni za siku za karibuni Le Pen, amekuwa nyuma ya Strauss-Kahn kwenye nafasi ya uraisi.

Makamu Mwenyekiti wa chama cha Kisoshalisti cha Strauss-Kahn na mshirika wake wa karibu, Jean-Marie Le Guen, amekiri kwamba huu ni wakati mgumu kwa chama chake, ambacho kimekuwa na ndoto ya kushinda uchaguzi ujao. Le Guen akizungumza na kituo kimoja cha televisheni nchini Ufaransa usiku wa jana alisema, "Tukio hili limetulemea vibaya. Ni wazi litakuwa na matokeo mabaya ya kisiasa ambayo kwa sasa hatuwezi kuyakisia. Tupo kwenye kipindi kigumu sana ambacho kinahitaji uvumilivu. Ni maisha ya Strauss-Kahn na heshima yake ndiyo iliyo kwenye hatari hivi sasa."

Hapa Ujerumani, ambako Strauss-Kahn alikuwa akielekea wakati wa kukamatwa kwake hapo jana, Waziri wa Fedha Wolfgang Schäuble amesema kwamba imebidi msaidizi wa Strauss-Kahn aje badala yake, lakini akakataa kusema lolote kuhusu kashfa inayomkabili Strauss-Kahn:

"Lazima tuangalie kila upande. Jambo hili linachunguzwa na litawekwa wazi huko New York. Kuhusu hilo siwezi kusema chochote. Kudhani tu mara nyingi huwa si sahihi."

Tayari IMF imeshamtangaza msaidizi wa Strauss-Kahn, John Lipsky, kukaimu nafasi ya meneja mkurugenzi. Ujerumani, ikiwa nchi inayoongoza kwenye mpango wa Umoja wa Ulaya na IMF kuyaokoa mataifa ya eneo la sarafu ya Euro yanayoporomoka kiuchumi, imekuwa ikifanya kazi kwa karibu sana na Strauss-Kahn.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFPE

Mhariri: Josephat Charo

 • Tarehe 16.05.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/11Ghn
 • Tarehe 16.05.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/11Ghn

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com