1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya wahamiaji wanaokwenda Ulaya kutoka Libya yaongezeka

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
17 Agosti 2021

Wataalam wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, IOM wasema licha ya vurugu nchini Libya kupungua katika mwaka huu, idadi ya wahamiaji wanaokwenda barani Ulaya imeongezeka maradufu ikilinganishwa na mwaka uliopita. 

https://p.dw.com/p/3z5id
NGO I Sea-Watch 3 rettet Migranten
Picha: Darrin Zammit Lupi/REUTERS

Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limesema watu wapatao 20,257 wamekamatwa baharini na kurudishwa Libya hadi sasa katika mwaka huu. Nchi hiyo ya Kaskazini mwa Afrika ni sehemu kuu inayotumiwa  kuanza safari na maalafu ya wahamiaji haswa kutoka Kusini mwa Jangwa la Sahara wanaojaribu safari za hatari za kuvuka bahari ya Mediterranea kwenda barani Ulaya. Wengi wao hujaribu kufika kwenye pwani ya Italia, safari ambayo inahusisha umbali wa karibu kilomita 300.

Afisa mmoja wa jeshi la wanamaji la Libya, akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake ameliambia shirika la habari la AFP kwamba kumekuwepo na ongezeko la asilimia 100 la watu waliotaka kuondoka kuanzia mwezi Januari hadi mwezi Julai mwaka huu ikilinganishwa na kipindi kama hicho mnamo mwaka jana.

Wahamiaji waliookolewa na meli ya uokozi ya Ujerumani Sea-Watch 3
Wahamiaji waliookolewa na meli ya uokozi ya Ujerumani Sea-Watch 3Picha: Darrin Zammit Lupi/REUTERS

Wakili Anwar al-Werfalli, mtaalamu wa sheria za uhamiaji, amesema kuongezeka kwa idadi ya wahamiaji haswa baada ya mapigano kusimamishwa nchini Libya hali inayoifanya nchini hiyo kuwa na utulivu wa kiasi fulani ndio sababu kuu inayowahimiza wahamiaji kutaka kufanya safari hizo za hatari za kuvuka bahari ya Mediterrania.

Mazungumzo ya amani yaliyodhaminiwa na Umoja wa Mataifa yalifanikisha makubaliano ya kusimamisha mapigano nchini Libya mnamo Oktoba mwaka jana. Makubaliano hayo yameheshimiwa kwa jumla, na serikali ya mpito ilianzishwa mnamo mwaka huu.

Kulingana na Shirika la IOM, njia kuu ya baharini ya inayozigawa Libya, Italia na Malta ndio ya hatari zaidi ulimwenguni. Takwimu za IOM zinaonyesha kuwa wahamiaji wasiopungua 57 walizama mwezi uliopita.

Nalo Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR, zaidi ya wahamiaji na wakimbizi 10,000 wameingia nchini Italia katika kipindi cha miezi minne ya kwanza ya mwaka huu wa 2021, hilo likiwa ni ongezeko la asilimia 170 kulinganisha na kipindi hicho hicho katika mwaka jana wa 2020.

Bango linalosisititiza kuacha kuwatesa watu waliozuiwa kwenye kambi za Libya
Bango linalosisititiza kuacha kuwatesa watu waliozuiwa kwenye kambi za LibyaPicha: David W Cerny/REUTERS

Wakili Anwar al-Werfalli, mtaalamu wa sheria za uhamiaji amesema wafanyabiashara haramu ya kusafirisha watu sasa wameongeza operesheni zao ili kufidia hasara waliyopata katika miezi mingi ya vizuizi vya kupambana na janga la Covid-19. Wahamiaji wengi ambao walilazimika kusimamisha mipango yao sasa wameanza tena shugfhuli za kutaka kuvuka bahari ya Mediterrania.

Miloud el-Hajj, profesa wa uhusiano wa kimataifa, ameeleza kwamba wafanyabiashara hao haramu waliutumia vibaya mzozo wa Libya, kwa kiwango ambacho nchi hiyo ikageuka na kuwa kitovu cha usafirishaji watu kinyume cha sheria.

Walinzi wa pwani wa Libya kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na shutuma za kuwatendea vibaya wahamiaji. Mwishoni mwa mwezi Juni, shirika la misaada la Ujerumani Sea-Watch lilichapisha picha za angani zilizoonesha meli ya walinzi wa pwani ya Libya ikifyatua risasi karibu mita mbili hadi tatu kuilenga boti iliyokuwa imewabeba wahamiaji karibu 50.

Walakini, Jumuiya ya Ulaya na Italia kwa miaka kadhaa ndio zilizokuwa zinafadhili, kuwafundisha na kuwapa vifaa walinzi wa pwani wa Libya kwa ajili ya kuwazuia wasafirishaji haramu wanaowapeleka wahamiaji barani Ulaya kwa kutumia boti za kujitengenezea.

Baadhi ya watu wanaojaribu kuvuka bahari ya Mediterrania kwenda bara Ulaya
Baadhi ya watu wanaojaribu kuvuka bahari ya Mediterrania kwenda bara UlayaPicha: (Hannah Wallace Bowman/MSF/SOS Mediterranee/AP Photo/picture alliance

Wanaokamatwa baharini na kurejeshwa Libya wanawekwa katika vizuizi ambapo wanateseka mno. Sheria ya kimataifa ya baharini inasema wale waliookolewa baharini wanapaswa kuteremshwa kwenye bandari salama, na Umoja wa Mataifa haufikirii kuwa bandari za Libya ni katika kundi hilo la bandari salama. Kwa upande wake mamlaka nchini Libya zinasema hawana rasilimali za kutosha na wafanyikazi kuweza kukabiliana na shida hiyo.

Chanzo://AFP