1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Janga

Shambulizi la anga lawaua watu tisa nchini Kongo

Lilian Mtono
3 Mei 2024

Shambulizi la anga limewaua karibu watu tisa hii leo, miongoni mwao watoto saba katika kambi ya wakimbizi wa ndani mashariki mwa mji wa Goma nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

https://p.dw.com/p/4fUXK
Shambulizi la DRC
Shambulizi la anga lawaua watu tisa katika kambi ya wakimbizi wa ndani nchini DRCPicha: Alain Uaykani/Xinhua/picture alliance

Haikujulikana mara moja aliyefanya shambulizi hilo. Mkuu wa wilaya ya Lac Vert ambako shambulizi hilo limefanyika, Dedesi Mitima, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba aliiona miili ya watoto saba na watu wazima wawili wanaume. 

Baadhi ya watu walijeruhiwa na idadi hiyo ya vifo huenda ikaongezeka, amesema Mitima. Jeshi la Kongo halikupatikana mara moja kuzungumzia shambulizi hilo.

Majeshi ya Kongo na Uganda yawauwa wanamgambo watano Beni

Hali hii imezua wasiwasi mkubwa kati ya jamii ya wakimbizi, ambayo imekasirishwa sana kuona wanakuwa wahanga hata mahali ambapo walitafuta hifadhi. Wakimbizi hao waliandamana asubuhi ya leo na polisi walipojaribu kuyachawanya kwa risasi za moto, mwanamke mmoja aliuawa.

Kwa kuwa mizinga ya jeshi la Kongo iko umbali wa mita chache tu kutoka kambi ya wakimbizi tangu mapigano yakaribie mji wa Goma, baadhi ya watu wanadhani huenda mashambulizi haya yalilenga maeneo haya, lakini kwa bahati mbaya yakaangukia katika makambi ya wakimbizi wa ndani.

Hata hivyo, kwa mara nyingine tena waasi wa M23 wamekanusha kuhusika na mashambulizi hayo na badala yake wametoa taarifa ya kuyalaani na kuvilaumu vikosi vya jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.