1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shalit kurejea nyumbani, Wapalestina 477 kuachiwa huru

18 Oktoba 2011

Awamu ya kwanza ya mpango huo inatarajiwa kuanza mnamo saa kumi na mbili alfajiri zaa eneo hilo la Mashariki ya kati.

https://p.dw.com/p/12tpa
Gilad Shalit.Picha: AP

Kwa mujibu wa msemaji wa Idara ya Magereza ya Israel, Sivan Weizman, misafara kadhaa ya magari yatakayowasafirisha wafungwa hao wa Palestina itapata idhini ya kuondoka pindi jeshi litakapoiamuru. Msafara mmoja wa magari yatakayowasafirisha wafungwa wa kike utaondokea gereza ya Sharon iliyoko katikati mwa Israel hadi eneo la kituo cha ukaguzi kilicho karibu na mji wa Ramallah. Msafara mwengine utatokea eneo la gereza la Ketziot lililoko kusini mwa Israel.

Mwiba mkali

Sakata hiyo imewatatiza waIsraeli kwa muda wa zaidi ya miaka mitano ambayo amekuwa akizuiliwa mwanajeshi wao, Gilad Shalit katika Ukanda wa Gaza. Aviva Shalit, mamake, Gilad Shalit anasisitiza kuwa siku ya leo ni ngumu.


Duru zinaeleza kuwa Misri ambayo ndiyo mpatanishi mkuu, itampokea Shalit kutoka mikononi mwa viongozi wa Hamas na kuwakabidhi viongozi wa Israel watakaowaachia huru sanjari, wafungwa wa Palestina katika maeneo kadhaa wanakozuiliwa.

Flash-Galerie Vorbereitungen für Gefangenenaustausch in Gaza
Wanaharakati waliosusia chakula ili kuwaunga mkono waPalestina wanaozuiliwa jela Israel.Picha: DW/Shawgy El-Farra

Itakumbukwa kuwa , Gilad Shalit aliye na umri wa miaka 25 alikamatwa mwezi wa Juni mwaka 2006 na wanamgambo waliolifikia kundi lao kwa kupitia mahandaki yanayotokea Palestina hadi Israel.

Operesheni hiyo ya kushtukiza ilisababisha vifo vya wanajeshi wengine wawili wa Israel waliokuwa pamoja na Gilad Shalit. Pindi baada ya kuachiwa, mwanajeshi huyo wa Israel atasafirishwa kwa ndege hadi kwenye kambi moja ya jeshi iliyoko katikati mwa Israel atakakolakiwa na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, viongozi wa serikalini pamoja na jamaa kabla ya kuelekea nyumbani kwake kaskazini mwa nchi.

Wakati huohuo, viongozi wa Hamas wanajiandaa kuwapokea kiasi ya waPalestina 295 kati ya kundi la 477 watakaoachiwa huru katika awamu ya kwanza ya mpango huo wa kubadilishana wafungwa. Ashraf Abu Zaid wa kundi la Hamas anasisitiza kuwa leo ni siku ya furaha kubwa.

Protestmarsch für die Freilassung des entführten israelischen Soldaten Gilad Shalit
Maandamano ya Ukingo wa MagharibiPicha: picture-alliance/dpa

Uhamishoni na Uhuru

Hata hivyo 41 kati ya kundi hilo la kwanza watalazimika kwenda uhamishoni katika mataifa ya kigeni. Duru zinaeleza kuwa uongozi wa mataifa Uturuki, Qatar na Syria wanajiandaa kuwapokea wafungwa hao watakaoenda uhamishoni baada ya kiongozi wa Hamas, Khaled Meshal, kukutanao nao mjini Cairo nchini Misri.

Kundi jengine la Wapalestina hao watapelekwa hadi maeneo ya Ukingo wa Magharibi watakakopokelewa na jamaa pamoja na Rais wa Palestina, Mahmoud Abbas ambaye ni hasimu mkubwa wa kisiasa wa viongozi wa kundi la Hamas.

Kwa mtazamo wa Wapalestina, wafungwa hao waliokuwa wakizuiliwa na Israel ni wa vita. Ifahamike kuwa Israel inawazuilia kiasi ya wafungwa 6,000 wa Palestina. Israel iliviondoa mwaka 2005 vikosi na raia wake kwenye Ukanda wa Gaza ila inaendelea kulidhibiti eneo la pwani baada ya mwanajeshi wao Gilad Shalit kukamatwa. Kulingana na WaIsraeli, tukio hili la leo linawachoma kwani idadi ya wafungwa wa Palestina wanaoachiwa huru ni kubwa.

Suala nyeti

Vyombo vya habari vya Israel vimekuwa vikiliangazia suala hilo tangu wiki moja iliyopita alipotangaza Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kuwa amefanikiwa kufikia makubaliano yatakayo muachia huru Gilad Shalit. Katika Ukanda wa Gaza, mabango yametundikwa kila mahali na siku ya leo ni kuu na mhadhara mkubwa umeandaliwa.

Israel Palästinenser Gaza Vorbereitung Gefangenaustauch Gilad Schalit palästinensische Häftlinge
Mabasi ya Israel yatakayowasafirisha wafungwa wa Palestina.Picha: dapd

Taarifa zinaeleza kuwa awamu ya pili ya kubadilishana wafungwa inatazamiwa kufanyika katia kipindi cha miezi miwili ijayo ambapo kiasi ya Wapalestina 550 wataachiwa huru. Jumla ya wafungwa 1027 wa Palestina wataachiwa huru kama ilivyoafikiwa katika mpango huo wa kubadilishana wafungwa.

Mwandishi: Mwadzaya, Thelma-RTRE/DPAE/AFPE