1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwelekeo ni upi baada ya makubaliano ya Brexit kuangushwa?

16 Januari 2019

Wabunge wa Uingereza Jumanne waliyakataa pakubwa makubaliano ya Waziri Mkuu Theresa May na Umoja wa Ulaya kuhusu Uingereza kujiondoa kutoka kwenye Umoja huo, jambo lililouvuruga mchakato wa Brexit.

https://p.dw.com/p/3Bc77
England Brexit Theresa May
Picha: Reuters TV

Hatua hiyo imepelekea kura isiyokuwa na imani kuwasilishwa, hatua ambayo inaweza kuiangusha serikali ya May. Wabunge walioyapinga makubaliano hayo ni 432 huku walioyaunga mkono wakiwa 202 pekee. Kushindwa kwa Waziri Mkuu huyo kulitarajiwa na wengi ingawa kiasi cha kura alizoshindwa nazo ni jambo ambalo limeuharibu uongozi wake unaosuwasuwa.

Kushindwa huku ni kwa kihistoria kwa kuwa ndiyo mara ya kwanza kwa serikali kushindwa kwa kiasi kikubwa cha kura katika bunge la Uingereza na kunafuatia msukosuko wa kisiasa wa zaidi ya miaka miwili ambapo May alijiwekea hadhi ya kisiasa kwa kuhakikisha amepata makubaliano ya Brexit. 

Jeremy Corbyn aliwasilisha mswada wa kutokuwa na imani na serikali ya May

Muda mfupi baada ya matokeo kutangazwa na spika John Bercow Waziri Mkuu May, alizungumza.

"Ahsante bwana Spika. Bwana Spika bunge limeshasema na serikali itasikiliza. Ni wazi kwamba bunge haliungi mkono makubaliano haya ila kura ya usiku wa leo haituambii bunge linaunga mkono hasa kitu gani, haituambii chochote kuhusu ni vipi au hata ikiwa linaunga mkono uamuzi wa Waingereza katika kura ya maoni iliyoamuliwa na bunge hili. Na watu hasa raia wa Umoja wa Ulaya ambao wamefanya makao yao hapa na raia wa Uingereza wanaoishi katika nchi za Umoja wa Ulaya, wanastahili kupata uwazi kuhusiana na maswali haya haraka iwezekenavyo," alisema May.

Großbritannien London - Jeremy Corbyn zu Parlamentsabstimmung
Kiongozi wa upinzani Jeremy Corbyn amewasilisha mswada wa kutokuwa na imani na MayPicha: Reuters

Mara tu baada ya May kuzungumza kiongozi wa upinzani Jeremy Corbyn alisema serikali yake imepoteza imani ya bunge. Wabunge Jumatano watapiga kura kuhusiana na mswada wake wa kutokuwa na imani na serikali aliouwasilisha. Iwapo serikali itapoteza kura hiyo, itakuwa na siku kumi na nne za kuyapindua matokeo hayo au iitishe uchaguzi wa mapema. Lakini inavyoelekea huenda Waziri Mkuu huyo akaponea kura hiyo labda tu wabunge kutoka chama chake cha Kihafidhina wamsaliti.

Waziri Kiongozi wa Scotland anataka kura mpya ya maoni kuhusu Brexit ifanyike

Raia wa Uingereza wanaounga mkono kusalia kwenye Umoja wa Ulaya walikuwa wakifuatilia matokeo yaliyoonyeshwa kwenye televisheni zilizokuwa nje ya bunge na wamefurahia kuangushwa kwa makubaliano hayo ya May.

"Nina furaha kwamba makubaliano yameangushwa. Lakini ni hatua ya kwanza tu. Tunachohitaji kwa sasa ni kura nyengine ya maoni. Katika kampeni iliyopita watu walidanganywa, nafikiri kwa sasa sote tunafahamu vyema na ni wakati wa kupata nafasi nyengine ya kupiga kura."

Theresa May und Nicola Sturgeon
Waziri Kiongozi wa Scotland Nicola Sturgeon ataka kura nyengine ya maoniPicha: picture-alliance/empics/J. Barlow

Waziri Kiongozi wa Scotland Nicola Sturgeon ni miongoni mwa waliopaza sauti zao baada ya kura hiyo na amemtaka Theresa May kuufutilia mbali mchakato wa Brexit na kuandaa kura ya pili ya maoni kuhusiana na suala hilo.

Serikali ya Uhispania nayo imeonya kwamba makubaliano waliyoyakataa wabunge wa Uingereza ndiyo yaliyokuwa bora zaidi na kwamba kuanzisha mazungumzo tena kuhusiana na Brexit ni jambo litakaloelekea katika hali ya hatari. Serikali hiyo ya Kisosholisti imesema makubaliano hayo yalikuwa yanatetea vyema maslahi ya pande zote mbili pamoja na haki za raia na wadau katika uchumi.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron naye ambaye alikuwa kwenye mkutano na maafisa wa Ufaransa alipoambiwa matokeo ya kura hiyo amesema, Uingereza ndiyo itakayokuwa imepoteza pakubwa wapo itaondoka katika Umoja wa Ulaya bila makubaliano.

Mwandishi: Jacob Safari/APE/Reuters