Schumacher atamba China | Michezo | DW | 02.10.2006
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Michezo

Schumacher atamba China

Bingwa mara saba wa mbio za magari,mjerumani M.Schumacher ameshinda jana mbio za Grand Prix huko China na kwa mara ya kwanza anaongoza katika kinyan'ganyiro cha kuania taji la dunia msimu huu.

Muivory Coast B.Sanogo apongezwa kwa bao lake :hamburg 1:cottbus 0

Muivory Coast B.Sanogo apongezwa kwa bao lake :hamburg 1:cottbus 0

Katika Bundesliga-Hertha Berlin, imerejea kileleni mwa ngazi ya Ligi kufuatia sare ya mabao 2:2 na Stuttgart.Mbali na kushinda mechi 2 kati ya sita msimu huu,Hertha,inaongoza orodha ya timu 5 zenye pointi kumi-kumi lakini kwa wingi wa magoli tu.

Hii haikuwahi kutokea mwanzoni mwa Bundesliga timu kukaribiana namna hivyo kileleni.Nuremberg,Werder Bremen,Schalke na mabingwa watetezi-Munich zote ziko nyuma ya Berlin baada ya mechi 6 kuchezwa.Msangao ulizuka jumamosi pale mabingwa Bayern Munich walipozabwa bao 1:0 na Wolfsburg na jana Schalke ikakumtwa mabao 3:1 na Bayer Leverkusen.

Katika Premier League-ligi ya Uingereza, Manchester United imerudi kileleni kufuatia ushindi wa mabao 2:0 nyumbani dhidi ya New Castle.Mabao yote 2 yalitiwa na Gunnar Solskjaer.Manchester United ina jumla ya pointi 16 na inaongoza kwa magoli tu mbele ya mabingwa Chelsea.Chelsea ilimudu sare tu bao 1:1 na Aston Villa.

Na katika la La Liga, huko Spian, mabingwa FC Barcelona walinguruma kwa mabao 3:1 mbele ya Athletic Bilbao .Real Madrid, ilipanda hadi ngazi ya tatu kutoka juu kwa kumudu suluhu ya bao 1:1 na Atletico Madrid.

Ama nchini Ufaransa, Olympique Lyon, ilishika usukani barabara mkononi kwa ushindi wa bao 1:0 dhidi ya Sochaux.

Katika changamoto za kombe la klabu bingwa barani Afrika,Orlando Pirates ya Afrika kusini ilipoteza nafasi chungu nzima nyumbani na sare ya 0:0 kati yake na Club Sportif Sfaxien ya Tunisia, haitatosha kuikatia tikiti ya finali ya kombe hili mwaka huu.

Hii pia ni mara ya kwanza kwa watunisia kushindwa kutia bao katika mapambano yao 13 ya champions League-kombe la klabu bingwa barani Afrika.Katika

Nusu-finali ya pili ilikuas kati ya Al Ahly ya Misri,mabingwa na ASEC Memosa ya Ivory Coast mjini Cairo.

Duru ya pili itachezwa Oktoba 14 huko Sfaxien nchini Tunisia.

AFRIKA KUSINI NA KOMBE LA DUNIA 2010:

Gharama za kujenga viwanja vipya na kuvikarabati vya zamani kwa kombe lijalo la dunia kwa Afrika kusini, zitafikia rand bilioni 8.352 na hii ni sawa na dala bilioni 1.077.Gharama hizo kwahivyo ni kubwa mara 3 kuliko ilivyokisiwa mwanzo na zaidi ya rand bilioni 3 ilizosema serikali ya Afrika kusini mwaka mmoja uliopita kuweka kando kwa matengenezo ya viwanja vya zamani.

Afrika kusini inahitaji viwanja 5 vipya kwa maandalio ya kombe la mashirikisho-Confederations Cup-kombe linalotangulia mwaka mmoja kabla Kombe la dunia hapo kati ya 2009.

Ni kati ya wiki iliopita tu, rais wa FIFA-shirikisho la dimba ulimwenguni-Sepp Blatter,aliishauri Brazil kwamba ikiwa kweli inataka kuandaa kombe la dunia 2014 baada ya Afrika Kusini,ianze sasa kujenga viwanja vipya.

Taarifa kutoka Rio de jeneiro, zinasema kipa wa Brazil Dida, ameamua kutoichezea tena timu ya Taifa –hii ni kwa muujibu wa Dunga,kocha wa Brazil alivyoarifu jana.

Dida ndie alielinda lango la Brazil katika kombe lililopita la dunia hapa Ujerumani.Dida alikaa langoni kwa mara ya kwanza 1997 pale Brazil ilipocheza na Bafana Bafana-Afrika Kusini.Kwa jumla, ameichezea Brazil mara 92 na alilinda pia lango la Brazil katika dimba la olimpik 1996 huko Atlanta na kumalizikia na medali ya shaba.

Taifa Stars, timu ya taifa ya Tanzania ikijiandaa kwa changamoto yake ya kuania tiketi ya finali ya kombe la Afrika la mataifa huko Ghana,2008 dhidi ya Msumbiji,ilipiamana nguvu mwishoni mwa juma na jirani Harambee Stars ambayo ina miadi na Angola.

Burundi ilikua uwanjani na Misri kuania tikiti za finali ya kombe la vijana la Afrika mwakani huko Kongo-Brazzaville.Misri ilishinda kwa bao 1:0.

Katika medani ya riadha, muafrika Kusini Hendrik Ramaala ameshinda mbio za nusu-marathon Great North Run, hii ikiwa ni mara ya 3 kushinda mbio hizo.Ramaala alimpiku muethiopia Dejene Berhanu aliekuja wapili.

Upande wa wanawake, ushindi lakini ulikwenda kwa muethiopia Berhane Adere,bingwa wa zamani wa dunia wa mbio za nusu-marathon.

Michael Schumacher wa Ujerumani anaelekea atastaafu msimu huu akiwa bingwa wa dunia wa mbio za magari za fomular one kwa mara ya 8 –hii ikiwa ni rekodi.

Bingwa wa dunia ,mspain Alonso alieanza akiwa usoni alimaliza wapili.Schumacher alianza nafasi ya 6,lakini aliibuka mwishoe wa kwanza.Hii ni mara ya kwanza msimu huu, kwa Michael Schumacher kuongoza mbele ya Alonso.Dereva huyu wa Ujerumani na bingwa mara 7 wa dunia, alijipatia jana huko China ushindi wake wa 91.

Endapo akitamba tena wiki ijayo huko Japan, basi hakuna atakaemzuwia asitoroke na taji la 8 msimu huu na kustaafu.

 • Tarehe 02.10.2006
 • Mwandishi Ramadhan Ali
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHd6
 • Tarehe 02.10.2006
 • Mwandishi Ramadhan Ali
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHd6