1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Schalke, Manchester United vitani leo.

26 Aprili 2011

Mechi za mkondo wa kwanza za nusu fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, UEFA, zinang'oa nanga leo usiku

https://p.dw.com/p/114FY
Raul Gonzalez kuongoza mashambulizi ya SchalkePicha: picture alliance / Pressefoto Ulmer

Schalke 04 ya ujerumani itawakaribisha nyumbani miamba wa uingereza, Manchester United, katika mchuano ambao wengi wanausubiri kwa hamu kujua ikiwa Schalke tena watasababisha mshangao mwingine.

Kikosi cha Sir Alex Ferguson, Manchester United, huenda kinaonekana kuwa bora kufuzu kwa fainali ya kivumbi hicho kwa mara ya tatu katika miaka minne, lakini kilibanduliwa nje na Bayer Leverkusen mnamo mwaka wa 2002 baada ya kuondolewa na borussia Dortmund katika fainali ya mwaka wa 1997.

Mabingwa hao wa Champions League wa mwaka 1999 na 2008 hawajawahi kushinda mechi za mtoano dhidi ya timu ya Ujerumani mara nne tangu kuanzishwa kwa ligi ya mabingwa mwaka 1992, na walishindwa katika nusu fainali msimu uliopita dhidi ya Bayern Munich.

United wanafahamu vyema kabisa umahiri wa ufungaji mabao wa mhispania, Raul Gonzalez, ambaye sasa anachezea Schalke 04 baada ya miaka 16 akiwa na Real Madrid na ambaye alifunga mabao mawili uwanjani Old Traford na kuwaondoa mashetani hao wekundu ambao walikuwa mabingwa watetezi wakati huo.

Manchester United vs. Chelsea
Wachezaji wa Manchester wakishangilia moja ya mechi walizoshindaPicha: dapd

Kocha wa Man United, Alex Ferguson, amesema kuwa mchuano wa leo utakuwa mgumu zaidi na ataupa uhumimu mkubwa.

Mwenyeji wake, Ralf Rangnick, naye amesema kuwa Schalke hawana shinikizo lolote wanapocheza na United, kwani wamefurahia kufika pale walipo na watajitahidi zaidi.

Wachezaji wa Schalke pia nao wamejawa na hamasa kubwa baada ya kuwapiku mabingwa watetezi Inter Milan na wamejiandaa kwa kibarua cha leo jinsi anavyoeleza mlinda lango Christoph Metzelder

Raul ni mfungaji bora wa Schalke akiwa na mabao matano msimu huu kwenye kivumbi hicho, huku naye Javier Hernandez akiwa mfungaji bora wa United akiwa na mabao manne kufikia sasa.

Mshindi wa nusu fainali hiyo atakabana koo na Barcelona au Real Madrid katika fainali itakayochezewa uwanjani Wembley mjini London Mei 28.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters

Mhariri: Miraji Othman