1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sarkozy bado mashakani

Admin.WagnerD4 Mei 2012

Siku mbili kabla ya duru ya pili ya uchaguzi wa raisi Ufaransa, kura za maoni zimempandisha kidogo Nicolas Sarkozy ingawa matumaiani yake yanafifia baada ya viongozi wa mirengo ya kulia na kati kukataa kumuunga mkono.

https://p.dw.com/p/14pT5
Mtetezi wa kiti cha urais, Nicolas Rakozy wa Ufaransa.
Mtetezi wa kiti cha urais, Nicolas Rakozy wa Ufaransa.Picha: reuters

Matokeo ya mwisho ya uchunguzi wa maoni ya wapiga kura yaliyochapishwa leo, yanaonesha kuwa bado ni mpizani wa Sarkozy, Francois Hollande, anayeongoza japo kwa upungufu wa alama 5 kutoka asilimia 10 alizokuwanazo wiki iliyopita.

Uchunguzi wa maoni uliofanywa tangu kufanyika kwa mdahalo wa televisheni kati ya Hollande na Sarkozy hapo Jumatano (Mei 2, 2012), unamuonesha Sarkozy akipanda kwa alama chache juu, ingawa si rahisi kwake kuziba pengo la tafauti ya kura zilizopo kati yake na Hollande.

Uchunguzi uliofanywa na taasisi za Ipsos na BVA umegundua kuwa uwezakano wa ushindi wa Hollande umeshuka kwa asilimia 1, kwa sasa kuwa na asilimia 52.5 kwa asilimia 47.5 za Sarkozy.

Uchunguzi mwengine uliofanywa na taasisi za CSA na Harris Interactive unaonesha kuwa uwezekano wa ushindi wa Hollande umeshuka kutoka alama 8 hadi 6 baada ya mdahalo, na kumfanya Hollande kuwa na asilimia 53 dhidi ya 47 za Sarkozy.

Taasisi nyengine ya uchunguzi wa maoni, TNS-Sofres, imeushusha uwezakano wa ushindi wa Hollande kwa alama 1.5 na kuupandisha wa Sarkozy hadi asilimia 46.5.

Bado Sarkizy hana nafasi ya ushindi

Lakini matokeo haya mapya ya uchunguzi wa maoni, bado hayampi nafasi yoyote Sarkozy, ambaye amejikuta akikosa uungwaji mkono wa waliokuwa wagombea muhimu katika duru ya kwanza.

Francois Bayrou (kushoto) na Francois Hollande.
Francois Bayrou (kushoto) na Francois Hollande.Picha: Reuters

Aliyekuwa mgombea wa mrengo wa kati, Francois Bayrou, amezidi kuyazamisha matumaini ya Sarkozy baada ya kutangaza kwamba yeye binafsi atampigia kura Hollande na kuwaacha wapiga kura wake waamue wenyewe.

Bayrou, aliyeshika nafasi ya tano kwenye duru ya kwanza ya uchaguzi akiwa na asilimia tisa ya kura, alimshambulia Sarkozy kwa kauli zake kazi juu ya masuala ya uhamiaji na Ulaya, zilizokusudiwa kuvuna angalau kura moja kwa kila tano ya zile zilizompigia mwanasiasa mwenye msimamo mkali wa mrengo wa kulia, Marine Le Pen, katika duru ya kwanza.

Hata Le Pen, anayepinga waziwazi wahamiaji alimuangusha Sarkozy wiki hii, baada ya kusema kwamba atatumbukiza karatasi tupu ya kura kwenye kisanduku, badala ya kumpigia mgombea yeyote kati ya Sarkozy na Hollande.

Lakini licha ya kuongoza kwenye kura za maoni, bado Hollande amesema kwamba hapuuzii uwezekano wa kushindwa kwenye kura ya hapo Jumapili, akitaja masuala ya ushiriki wa wapiga kura, wapiga kura watakaohamishia kura zao na hata wale ambao watatumbukiza karatasi tupu kwenye masanduku na uwezo binafsi wa Sarkozy, kama mwanasiasa.

Hollande amekiambia kituo cha habari cha RTL, kwamba haudharau uwezo wa Sarkozy kufanya siasa za kufa na kupona, akirejelea kuwa kosa la Sarkozy lilikuwa ni kumdharau yeye.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Othman Miraji