Sarkozy ataka mageuzi katika Umoja wa Ulaya
2 Desemba 2011Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa amesisitiza ulazima wa kuleta mageuzi nchini mwake na katika Umoja wa Ulaya kwa jumla.
Sarkozy amesema Umoja wa Sarafu ya Euro unahitaji udhibiti wa bajeti na utaratibu wa adhabu kwa nchi zinazokiuka nidhamu ya bajeti. Ameyasema hayo katika hotuba aliyoitoa mjini Toulon kwa watu 5,000 wanaomuunga mkono.
Kiongozi huyo wa Ufaransa pia ameeleza kuwa anakusudia kuujadili mpango wa pamoja wa Ufaransa na Ujerumani wa kuukabili mgogoro wa madeni, atakapokutana na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel mjini Paris jumatatu ijayo.
Mpango huo pia unahusu kuleta mabadiliko katika Mkataba wa Umoja wa Ulaya.
Sarkozy amesema yeye pamoja na Kansela Merkel watauwasilisha mpango huo kwenye mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Ulaya utakaofanyika wiki ijayo.
Rais Sarkozy pia amewataka wananchi wake wawe tayari kwa hatua za kubana matumizi katika sekta ya umma.