Sarkozy aonya Ulaya yakabiliwa na mzozo
17 Januari 2012Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy ameonya kuwa Ulaya inakabiliwa na mzozo mkubwa, na inapaswa kutafuta njia mpya ya kukuza uchumi. Sarkozy amesema baada ya mazungumzo na waziri mkuu wa Uhispania Rajoy mjini Madrid kuwa mataifa ya Ulaya yanapaswa kupunguza matumizi, kupunguza nakisi na kutatua matatizo ya ndani ya ushindani. Matamshi yake yamekuja wakati benki kuu ya umoja wa Ulaya imesema kuwa imenunua mara tatu zaidi dhamana za eneo la mataifa ya euro hadi kiasi cha euro bilioni 3.76 wiki iliyopita kuweza kuzuwia gharama za ukopaji. Ufaransa , ilipuuzia kupunguziwa alama tatu za A katika uwezo wa kukopa, na kuuza kiasi cha euro bilioni 8.6 katika deni la muda mfupi jana Jumatatu kwa riba ya chini kuliko kabla ya kupunguziwa kiwango hicho. Wakati huo huo , shirika la kuweka viwango la Standard and Poors imeshusha kiwango cha mfuko wa uokozi wa mataifa ya Ulaya EFSF kwa alama moja hadi A mbili. S&P imesema hata hivyo kuwa , itarejesha kiwango cha A tatu , iwapo mfuko huo utapata dhamana zaidi.